Kitu kimoja unachopaswa kujua na kukizingatia kila siku ni kwamba hasira ni usumbufu.

Unapokuwa na hasira, unahamisha umakini wako kutoka kwenye mambo muhimu na kuupeleka kwenye mambo ambayo siyo muhimu.

Na wale ambao wanataka kunufaika na wewe kwa namna fulani au wanaotaka ukosee, huwa wanatumia mbinu ya kuamsha hasira zako, na ukiingia kwenye mtego huo unaumia huku wao wakishinda.

Hivyo wajibu wako mkubwa ni kuhakikisha hasira haikutawali kwa namna yoyote ile, bila ya kujali ni kitu gani kimetokea au kinaendelea.

Dhibiti sana hasira zako, kwa sababu hizo zikishakuwa juu, uwezo wako wa kufikiri kwa usahihi unashuka na inakuwa rahisi kwako kufanya kilicho sahihi.

Hasira siyo mbinu wala mkakati utakaokuwezesha kupata au kushinda chochote. Bali hasira ni usumbufu ambao utakuondoa kwenye lengo kuu.

Pia wajue wale waibuaji wa hasira ndani yako, wale wanaokutega ili ukasirike na uchukue hatua ambazo zitapelekea ufanye makosa. Ukishawajua watu hawa, usiwape nafasi ya kukusumbua kabisa.

Waswahili wanasema hasira hasara, tunaongeza mkazo kwa kusema hasira ni usumbufu, kaa nazo mbali.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha