Tabia ya kuahirisha mambo ni moja ya tabia zinazowazuia watu wengi kufanikiwa.
Kuweka malengo na mipango ya mafanikio ni rahisi sana, lakini inapofika wakati wa kutekeleza kile ulichopanga, ndipo tabia ya kuahirisha inapoingia na mtu kujiambia utafanya baadaye au utafanya ukiwa tayari.
Sasa tumekuwa tunailaumu sana tabia ya kuahirisha mambo, kwamba ndiyo kikwazo kwetu.
Lakini unapoangalia kwa undani na kwa makini, unagundua tatizo siyo tabia ya kuahirisha, bali tatizo ni hamasa.
Kuelewa hili vizuri, angalia mfano huu. Kuna kazi unatakiwa kuikamilisha ndani ya mwezi mmoja unaokuja, kadiri siku za kuikamilisha zinavyokuwa nyingi, ndivyo unavyokuwa unaahirisha kuifanya.
Ukijiona una siku 30 za kufanya kitu, unajiambia siku ni nyingi na hivyo inakuwa rahisi kuahirisha. Unakuja kustuka siku 20 zimebaki, unajiambia bado muda upo. Zinabaki siku 10, unaanza kupunguza kuahirisha. Zinabaki siku 5 na hapo sasa kuahirisha hakufai. Na zinapobaki siku 2 au 1 ya kukamilisha jambo, hutafanya chochote zaidi ya kukamilisha jambo hilo.
Kadiri siku zinavyopungua, ndivyo hamasa kufanya kitu inavyokuwa kubwa na tabia ya kuahirisha inavyopungua.
Ndiyo maana nakuambia tatizo lako siyo tabia ya kuahirisha mambo, bali kukosa msukumo na hamasa wa kufanya jambo sasa badala ya baadaye.
Unaweza kutegemea msukumo wa nje kama unaweza kuupata, au kutengeneza mwenyewe msukumo wa ndani.
Jinsi ya kutengeneza msukumo wa ndani, ahidi kitu ambacho kitakusukuma sana na kama utashindwa basi kitakuumiza. Mfano kuna kazi unapaswa kuikamilisha ndani ya siku 30, waambie wahusika utakamilisha ndani ya siku 10 na kama utashindwa ndani ya siku hiyo basi usilipwe au upewe adhabu.
Kwa kutengeneza msukumo ndani yako, tabia ya kuahirisha inakaa pembeni kabisa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,