Kila mtu amekuwa anatafuta njia rahisi ya kuweza kupata fedha na mafanikio bila ya kufanya kazi kabisa. Na hili limewafanya watu wengi kuhangaika na mambo wasiyoyajua na kupoteza muda wao mwingi huku wasipate kile wanachotaka.
Rafiki, kama unataka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako, kama unataka kupata chochote kile unachotaka, kwanza anza kukimbizana na kitu hicho, badala yake weka mkazo kwenye kuwasaidia wengine. Jipoteze kwenye kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi, kwenye kutoa thamani zaidi kwa wengine, na moja kwa moja maisha yako yatakuwa bora, utapata kila unachotaka kupata.
Unapojipoteza kwenye kuwasaidia wengine, unapojitoa kuongeza thamani zaidi kwenye maisha ya wengine, hilo linakuja kukulipa zaidi. Kwa sababu hakuna thamani inayokwenda bure, dunia ina tabia ya kulipa kila kinachofanywa na mtu. Hivyo unapotoa thamani zaidi, dunia inakulipa thamani zaidi.
Kwa upande wa pili, achana kabisa na njia za mkato za kufanikiwa, epuka sana zile njia ambazo watu wanakuambia ni rahisi, utapata unachotaka bila ya kuweka kazi. Hizo siyo njia sahihi, zitakupotezea muda wako na hata fedha zako pia.
Kumbuka, utaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako kama utaweza kuwasaidia wengine kupata kile wanachotaka.
Hivyo kama unataka fedha, acha kujiangalia wewe unapataje fedha zaidi badala yake angalia ni watu gani unaoweza kuwasaidia kupata fedha zaidi. Kama umeajiriwa angalia ni kwa namna gani unaweza kumsaidia mwajiri wako kupata fedha zaidi. Kama unafanya biashara angalia ni kwa namna gani unaweza kuwasaidia wateja wako kupata fedha zaidi. Na watu hao wakipata fedha zaidi basi na wewe unapata fedha zaidi.
Hakuna njia nyingine, tofauti na hiyo ambayo ni ya uhakika kwako kufanikiwa. Hivyo ishi kwa msingi huo, msingi wa kukazana kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi na hilo kuleta matokeo bora kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,