Upo usemi unaosema kwamba ukipigana na nguruwe, wote mtachafuka matope, wakati wewe itakuwa kadhia kwako, nguruwe atakuwa anafurahia hali hiyo.

Maana rahisi ya usemi huu ni kwamba, mtu yeyote unayegombana, kubishana au kushindana naye, unajishusha kwenye viwango vyake. Na hata kama utashinda chochote unachopambana naye, kushiriki kwako kwenye mapambano yako kunakushushia hadhi yako.

Hivyo kuwa makini sana usiwe mtu wa kuanzisha au kuingia kwenye ugomvi, ubishi au ushindani na wengine. Hata kama una uhakika wa kushinda, lakini ushiriki wako utakuacha wewe na doa.

Na kikubwa zaidi, kumbuka hakuna mtu anayefanana na wewe, hakuna anayefikiri kama wewe, hakuna mwenye uwezo kama ulionao wewe. Hivyo unaposhindana na mwingine kwa namna yoyote ile, unatoka kwenye viwango vyako na kwenda kwenye viwango vya mwingine, ambavyo mara nyingi huwa ni viwango vya chini kuliko vyako.

Weka nguvu zako zote kwenye kuwa bora zaidi leo kuliko ulivyokuwa jana, kazana kupiga hatua zaidi ya pale ulipo sasa na waache wengine wakazane na mambo yao.

Usiwe mtu wa kuanzisha ugomvi, ubishi au ushindani, na wengine wanapokutega ili uingie kwenye vitu hivyo, kuwa mjanja na jitoe haraka sana kabla hujaleta madhara makubwa kwako.

Hakuna cha maana utakachopata kwenye ugomvi, ubishi na ushindani, achana kabisa na vitu hivyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha