Unapoanza kufanikiwa kwenye maisha yako, utakaribisha changamoto na usumbufu wa kila aina kutoka kwa watu mbalimbali.
Wapo ambao watakuiga, watafanya kile unachofanya na kutaka kufanikiwa kama wewe. Hawa wanaweza kukufanya usumbuke, uone kwamba mafanikio yako yapo hatarini na ushindani utakuwa mkubwa. Lakini watu wa aina hii hawapaswi kukusumbua hata kidogo, mafanikio huwa yanakwenda kwenye kitu halisi na siyo cha kuiga. Kama utaendelea kufanya kilicho sahihi, kama utaendelea kujisukuma kuwa bora zaidi, hakuna atakayeweza kukusumbua kwa kukuiga.
Wapo watu ambao watajifanya kuwa wewe ili wanufaike na mafanikio yako. Hawa ni tofauti kabisa na wanaokuiga, hawa wanajifanya ni wewe na kuwalaghai watu waende kwao kwa kuwafanya waamini wewe. Watu hawa wanaweza kuwalaghai baadhi ya watu, lakini safari yao haitakuwa ndefu kwa sababu mafanikio huwa hayaji kwa njia zisizo sahihi. Mafanikio yanakuja kwa njia za uaminifu na uadilifu, kwa kujenga sifa sahihi ambayo watu wanaiamini. Kwa anayelaghai, mwisho wake upo karibu.
Kuna ambao watakuambia bila wao usingefanikiwa, hawa ni wale wanaoamini walileta mchango mkubwa kwenye mafanikio yako, na hivyo kutaka uwajali kwa namna wanavyotaka wao. Watu hawa wanakuwa hata hawajaleta mchango mkubwa kiasi wanachosema, lakini kidogo walichofanya watakikuza na kuonesha kwamba wamekutoa wao, na usipofanya wanachotaka wao, basi una kiburi au umewasahau baada ya kufanikiwa. Hawa pia wasikusumbue, wewe fanya kile ambacho ni sahihi na siyo ambacho watu wanakutaka ufanye kwa sababu tu walikusaidia huko nyuma.
Na mwisho kuna ambao watakuja kwa lengo la kukuibia, iwe ni kwa kukulaghai au hata kwa kuanzisha kesi ya madai. Hawa unapaswa kuwa makini na kuhakikisha kila wakati unafanya kilicho sahihi.
Unayataka mafanikio makubwa, lakini mafanikio haya yanakuja na changamoto zake, hivyo zijue na jiandae kuzikabili ili zisiwe kikwazo kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,