Kuna mambo huwa yanaweza kutokea, yanatufanya tujiulize kama kweli dunia ina huruma au inatujali sisi ambao tupo hapa duniani.

Mambo hayo wakati mwingine yanatufanya kama kuna Mungu au nguvu kubwa inayoangalia mambo yanavyokwenda duniani na kwa nini iruhusu baadhi ya mambo kutokea, ambayo yanaonekana kabisa ni ya mateso kwa wasiostahili.

Leo nakuandikia, tujadili kidogo kuhusu dunia kutokuwa na huruma.

Hii ni dhana ambayo tumejipoteza nayo, kwa sababu sijui ni nani aliyetuambia kwamba dunia inapaswa kuwa na huruma.

Kwa sababu dunia haijali kuhusu uwepo wako, dunia inajiendesha kwa kanuni za asili, ambazo zinafanya kazi bila ya kujali kama wewe upo au haupo.

Swala anakula majani, simba anakula swala, hivyo ndivyo asili ilivyo. Haijalishi swala atafanya maombi kiasi gani, haitamzuia simba kumla anapokutana naye akiwa na njaa. Hakuna swala la huruma hapo, ni asili inafuata mkondo wake.

Kuna watu wanazaliwa na kufa ndani ya siku moja, wengine wanaishi mpaka ujanani, wengine uzeeni, hakuna swala la usawa au kukosa usawa hapo (japo kuna mambo tunafanya kuchagia), dunia inajiendesha yenyewe.

Hivyo basi, ni wakati wa sisi kuacha kujiuliza kama dunia ina usawa au haina na kuanza kuishi kwa kanuni za asili. Tujue jinsi ambavyo dunia inajiendesha kwa kanuni zake, na kufuata hizo, na kwa hakika maisha yetu yatakuwa bora. Hatutalalamikia chochote, tutapokea kila kinachokuja mbele yetu kama kinavyokuja na kukitumia kama inavyofaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha