Nimewahi kukueleza thamani ya ushauri wa bure, ambao watu wamekuwa wanakupa au unajitolea kuwapa watu wengine. Kwamba thamani ya ushauri huo ni sifuri na utakugharimu sana pale ambapo utaanza kuufanyia kazi.

Leo nakwenda kukupa upande wa pili wa vitu vya bure au rahisi. Upande huo ni kwenye biashara yako.

Wafanyabiashara wengi wasiokuwa na uelewa sahihi wa kukuza biashara zao, huwa wanakimbilia njia rahisi ya kutoa vitu vya bure au kupunguza bei.

Ni kweli njia hiyo inaweza kukuletea wateja wengi na wa haraka. Lakini wateja wanaokuja kwa njia hiyo huwa siyo wateja bora sana ambao unaweza kujivunia kuwa nao kwenye biashara yako.

Wengi huwa ni wateja wasiojali thamani na wasio tayari kulipa, wao wanawinda vitu vya bure na rahisi.

Hivyo epuka sana kuijengea biashara yako picha kwamba ni ya vitu vya bure au vya bei rahisi. Kwa sababu watu huwa wanalinganisha thamani na bei. Kama kitu ni rahisi sana, wanaojali thamani watanona hakina thamani sahihi.

Na pale unapotoa kitu bure, watu wanakiona hakina thamani kabisa.

Ufanye nini?

Cha kufanya anza na wateja unaowalenga, si unakumbuka biashara yako hawezi kuwahudumia kila aina ya wateja? Hivyo basi chagua unalenga wateja wa aina gani, wenye shida au uhitaji gani.

Ukishajua wateja wako na uhitaji wao, kazana kuwapa thamani ambayo inawafaa kweli. Na wanapoipata thamani, watu wanakuwa tayari kulipa kiwango sahihi, siyo bure na wala siyo rahisi.

Jambo hili linahitaji kazi, linahitaji uvumilivu na kazi ya hali ya juu, wengi hawapo tayari kwa hayo ndiyo maana wanakimbilia njia ya mkato.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha