Rafiki yangu mpendwa,

Sehemu kubwa ya watu hawapendi kazi wanazozifanya. Haya ni matokeo ambayo yamekuwa yanadhibitishwa na tafiti mbalimbali ambazo zinafanywa maeneo ya kazi. Wengi wanafanya kazi ili tu kupata fedha, lakini siyo kitu wanachopenda kufanya.

Lakini kikubwa cha kushangaza ni kwamba wengi wamenasa kwenye kazi hizo, licha ya kutokuzipenda kazi hizo, bado hawawezi kuziacha kwa sababu ndiyo tegemeo lao kwenye kuingiza kipato. Na kama hiyo haitoshi, watu hao pia wanakuwa na madeni makubwa ambayo wameingia kwa kutegemea kazi hizo.

Wapo ambao wanakuwa wamekopa magari, nyumba na matumizi mengine kiasi kwamba mishahara yao ina makato makubwa na kile wanachopokea hakiwatoshelezi kuendesha maisha yao.

Hivyo hapo mtu anakuwa kwenye mtego mara tatu, kwanza ni kwa kufanya kazi asiyoipenda, pili kwa kutokuwa na kipato kinachotosheleza na tatu ni kukosa uhuru wa muda wake, kwa sababu kazi inamhitaji na hawezi kupangilia maisha yao wanavyotaka wao wenyewe.

Wengi ambao wamejikuta kwenye hali hii wamekata tamaa, wakiamini hakuna namna wanayoweza kutoka kwenye hali hiyo, hivyo wanaendesha maisha yao wakiwa hawana matumaini mapya na makubwa ya kuweza kutoka pale walipokwama.

 

Vicent Pugliese ni mpiga picha ambaye alianza maisha yake kwa mtindo kama huo, alikuwa ameajiriwa na gazeti la michezo na kazi yake ilikuwa kupiga picha. Alijikuta ameshaingia kwenye maisha ya madeni na kipato kutokutosheleza. Lakini baada ya kupata maarifa sahihi, aliweka nia ya kuondoka kwenye ajira na madeni hayo na kupata uhuru kamili wa maisha yake.

Vicent anatushirikisha hadithi kamili ya maisha yake, jinsi alivyotoka kwenye utumwa wa ajira na madeni mpaka kufikia uhuru kamili wa maisha yake. Anatushirikisha hatua kwa hatua kwenye kitabu chake kinachoitwa FREELANCE TO FREEDOM; The Roadmap for Creating a Side Business to Achieve Financial, Time and Life Freedom.

Zipo hatua tano ambazo Vicent anasema mtu yeyote anaweza kupiga na kuweza kutoka kwenye utumwa na kwenda kwenye uhuru. Hapa tunakwenda kujifunza hatua hizo tano.

HATUA YA KWANZA; KUTORIDHIKA NA AJIRA.

Hatua ya kwanza ya kuelekea kwenye uhuru ni kugundua kwamba tayari upo kwenye utumwa. Na hilo linakupa hasira na kutokuridhika na hali uliyonayo, na kujiambia kwamba mambo yanapaswa kuwa tofauti na yalivyo sasa.

Hii ni hatua ambayo asilimia kubwa ya watu wapo, lakini cha kushangaza hakuna hatua wanazochukua kutoka hapo.

Mfano tafiti zinazofanywa zinaonesha zaidi ya asilimia 80 ya waajiriwa hawapendi kazi zao, siku za jumatatu ni siku mbaya sana kwa wengi na siku za ijumaa ni siku za furaha kwa waliowengi.

Watu wanaenda kazini kusukuma tu siku, lakini siyo kwa sababu wana msukumo mkubwa ndani yao wa kwenda kufanya kitu cha tofauti.

Wengi katika hatua hii wanakuwa na madeni makubwa, wakipokea kipato wanalipa sehemu ya madeni, kinaisha haraka halafu wanarudi kukopa tena. Wengi wanakuwa na ndoto kubwa za maisha yao, lakini kwa mazingira waliyopo wanakuwa wanajiambia hawawezi kuzifikia.

Huenda na wewe upo kwenye hatua hii, kama ndiyo basi endelea kusoma, maana kuna hatua za kukutoa hapo ulipo sasa.

SOMA; Hizi Ndio Mbinu Anazutumia Mwajiri Wako Kuhakikisha Unaendelea Kuwa Mtumwa Wake.

HATUA YA PILI; BIASHARA YA PEMBENI.

Hapa unakuwa umechoshwa sana na hatua ya kwanza, na kuamua kwamba hutakubali maisha yako yaendelee hivyo. Unaweka pembeni kuwalaumu wengine na kuamua kushika hatamu ya maisha yako.

Hapa unaanzisha biashara ya pembeni huku ukiendelea na kazi yako.

Sasa hatua hii ni ngumu sana, kwa sababu inakutaka utoe kafara vitu vingi. Wakati wafanyakazi wenzako wanapumzika na kwenda kwenye starehe mbalimbali, wewe unakwenda kufanya kazi kwenye biashara yako. Wakati wale anaokuzunguka wananunua vitu visivyo na umuhimu kwa mkopo, wewe unaweka nguvu na kila fedha uliyonayo kwenye kukuza biashara yako.

Hii ni hatua ambayo unaamsha ndoto ambazo ulikuwa umezizika, unaanza kufanya vile vitu ambavyo umekuwa unapenda na kutoa thamani kwa wengine.

Hatua hii pia ni ya kujifunza kwa maumivu, kujifunza kwa kukosea kwa hatua mbalimbali unazochukua. Utashindwa sana kwenye hatua hii, utaangushwa na kukatishwa tamaa. Lakini kama utaweza kuvuka hatua hii, utafika kwenye uhuru.

HATUA YA TATU; KUWA FRILENSA.

Baada ya kuanzisha biashara ya pembeni, ambayo ulianza kidogo na kujifunza mambo mengi kwa kukosea, unakwenda hatua ya tatu pale ambapo unakuwa unaingiza kipato kupitia biashara yako hiyo ya pembeni. Kwenye hatua hii, biashara yako ya pembeni imeshaota mizizi, umeshakuwa na wateja ambao wanakutegemea uwahudumie.

Kwenye hatua hii, zaidi ya asilimia 50 ya kipato unachohitaji ili kuendesha maisha yako inatoka kwenye biashara yako. Hapa unakuwa umeanza kunusa harufu ya uhuru na kuanza kufikiria kuondoka kwenye ajira yako ambayo inakubana.

Kwenye hatua hii, biashara yako ya pembeni inakua kwa kasi na kazi yako inakuwa kikwazo kwenye ukuaji zaidi wa biashara yako. Hapa majukumu ya kazi yako yanaingiliana na majukumu ya biashara na hivyo unafikiria kuachana na kazi ili kuweka nguvu zako zote kwenye kukuza biashara yako.

Kwenye hatua hii pia msongo unapungua, umeanza kulipa madeni unayodaiwa na hukopi tena, una akiba ambayo inakupa usalama na uhakika kwamba lolote litakalotokea basi una uwezo wa kulikabili. Kwa hatua hii, mambo yanaonekana kwenda vizuri, lakini bado unakuwa hujafikia uhuru kamili.

HATUA YA NNE; MAISHA YA UHURU.

Hii ni hatua ambayo maisha yako yapo huru, unaamka asubuhi na kuamua ufanye nini siku hiyo, hakuna mtu anayekulazimisha kufanya chochote. Haupo tena kwenye ajira na biashara yako inakwenda vizuri sana. Hakuna mtu yeyote anayekudai na una muda wa kutosha kwa ajili ya mambo yako muhimu na wale muhimu kwako.

Kwenye hatua hii pia unakuwa na afya bora kwa sababu una uhuru wa kuchagua ule nini na kwa wakati gani, na muda wa kufanya mazoezi na mambo mengine ya kiafya unapanga mwenyewe na siyo kutafuta kama unapokuwa umebanwa na ajira.

Kwenye hatua hii pia una nguvu kubwa ya kuchagua aina gani ya wateja unaofanya nao kazi. Kama kuna wateja ni wasumbufu unaacha kuwapa huduma zako na kuchagua wateja wachache ambao unawahudumia vizuri na wanathamini kile unachofanya.

Kwenye hatua hii pia unakuwa na akiba na uwekezaji ambao unayawezesha maisha yako kwenda hata kama huna kipato cha moja kwa moja kutoka kwenye biashara zako.

Hakuna chochote ambacho kinakuwa kikwazo kwako kwenye hatua hii, kwa sababu hata mteja mmoja akiondoka, unauwezo wa kuongeza wateja zaidi.

SOMA; Hatua Nane Za Kutengeneza Biashara Inayokupa Uhuru Mkubwa Na Unayoweza Kuiuza.

HATUA YA TANO; KILA SIKU NI SIKU YA UHURU.

Kwenye hatua ya nne, japo unakuwa kwenye uhuru, lakini zipo siku ambazo unasukumwa kufanya vitu ambavyo hutaki kufanya. Hasa pale ambapo biashara inakuwa inakutegemea kwa maeneo fulani.

Hatua ya tano ni hatua ya uhuru kamili, ambapo kila siku kwako ni siku ya uhuru. Unaweza kuchagua kujipa likizo ya mwezi mzima na ukasafiri kwenda popote dunia bila ya kujali gharama au kipato.

Hapa unakuwa umeacha kuwa frelensa na umekuwa mjasiriamali, ambapo unakuwa umeweza mfumo mzuri wa kuendesha biashara yako ambao unaweza kufanya kazi hata kama wewe haupo.

Hii ni hatua ambayo kila mtu anatamani kuifikia, iwe anaanzia kwenye ajira au biashara. Ni hatua ya maisha ya uhuru kamili, uhuru wa muda, uhuru wa fedha, uhuru wa eneo unalopatikana. Kwa kifupi, hakuna chochote kinachoweza kukuzuia, kwa sababu fedha siyo tatizo tena na hata biashara yako haikutegemei wewe moja kwa moja.

Rafiki, hizi ndizo hatua tano za kutoka kwenye ajira na madeni mpaka kufikia biashara na uhuru kamili wa maisha.

Yapo masomo mengi ambayo Vicent ametushirikisha kwenye kila hatua ya kuelekea kwenye uhuru, vitu muhimu tunavyopaswa kuzingatia kwenye kila hatua. Tutajifunza hayo kwa kina kwenye makala ya TANO ZA JUMA hili la 35. Usikose makala hiyo, kwa sababu utakuwa ufunguo muhimu kwako kuelekea kwenye uhuru kamili wa maisha yako.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

WhatsApp Image 2019-07-13 at 18.40.50