“The rational soul is stronger than any kind of fortune—from its own share it guides its affairs here or there, and is itself the cause of a happy or miserable life.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 98.2b
Hongera sana mwanamafanikio kwa nafasi hii nzuri sana tuliyoipata leo.
Ni siku bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari ROHO IMARA NI BORA KULIKO BAHATI NZURI…
Kama kuna kitu kimoja ambacho kile mmoja wetu anapaswa kukifahamu mapema kabisa kabla hajaingia kwenye kitu chochote ni kwamba mambo yatakwenda kuwa magumu, tena sana.
Kabla hujaingia kwenye ajira, lazima ujue kwamba kuna wakati mambo yatakuwa magumu sana kwenye ajira hiyo, kutokuelewana na wengine, kipato kutokutosha, majukumu mengi kuliko muda ulionao na hata kupingwa na wengine.
Kabla hujaingia kwenye biashara lazima ujue kwamba kuna wakati mambo yatakuwa magumu sana. Kuna wakati wateja watakuwa hawanunui licha ya kukuahidi kununua, wengine watakuja kwako na malalamiko, wengine wataiga biashara yako na kupunguza bei sana ili kuchukua wateja wako, utapingwa na kukosolewa, utatapeliwa na kuibiwa na huenda biashara hiyo ikashindwa kabisa na hivyo kuhitaji kuanza upya.
Kabla hujaingia kwenye mahusiano ya aina yoyote na mtu mwingine, lazima ujue na kukubali kwamba kuna wakati mahusiano hayo yatakuwa magumu sana. Kuna wakati hamtaelewana, kuna wakati mtataka vitu tofauti na hivyo kuibua mgogoro, kuna wakati utaeleweka vibaya kwa ulichosema au kufanya.
Kama unaingia kwenye jambo lolote ukifikiria kwamba kila kitu kitakwenda kama ulivyopanga, basi wewe ni mchanga kabisa kwenye safari hii ya mafanikio na unajiandaa kuumia na kuangushwa.
Unakuwa unategemea zaidi bahati ya nje badala ya kutegemea uimara wa ndani.
Unachohitaji ili kuvuka magumu mengi utakayokutana nayo kwenye kila eneo la maisha yako siyo bahati, bali uimara wa ndani.
Unapokuwa imara ndani, siyo tu unaweza kukabiliana na kila ugumu, bali pia unaweza kugeuza kila ugumu kuwa na manufaa kwako.
Hivyo weka juhudi katika kuboresha uimara wako wa ndani, weka juhudi katika kuimarisha fikra zako, hisia zako na uvumilivu wako.
Jiweke kwenye zile hali ambazo zinaweza kutokea hata kabla hazijatokea, hivyo zinapotokea hujikuti kwenye mstuko au mshangao, maana ni kitu ulitegemea kitokee.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuboresha uimara wako wa ndani ili uweze kukabiliana na kila ugumu badala ya kutegemea bahati.
#NidhamuUadilifuKujituma #AfyaUtajiriHekima #KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1