Msimamo wetu kwenye kisima cha maarifa ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.

Kwamba chochote tunachofanya, tunapaswa kukifanya kwa kutoa huduma bora kwa wengine, kukipenda na kuwapenda wale ambao tunawahudumia. Tukifuata msimamo huu, tutaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yetu.

Kuna huduma iliyo kuu, huduma ambayo ukiitoa unaongeza thamani kubwa kwa wengine na kuacha alama kubwa kwenye maisha yao.

Huduma hiyo ni kuwafundisha wengine kugundua ukweli, ambacho ndiyo kitu pekee kinachoweza kuwaweka huru na wenye furaha.

Tunajua kabisa kwamba ukweli ndiyo unaowaweka watu huru, na hivyo wale ambao wanataka kuchukua uhuru wa wengine, kitu cha kwanza wanachokifanya ni kuhakikisha hawaupati ukweli.

Hivyo wewe unapokuwa mtu wa kuwasaidia wengine kuuona ukweli, unakuwa umewapa kitu kikubwa sana, unakuwa umemulika njia yao ya kuelekea kwenye uhuru, furaha na mafanikio makubwa.

Kwa kazi au biashara yoyote ile unayofanya, kuna ukweli ambao watu wamefichwa kwa muda mrefu. Wakati mwingine ukweli huo hata haujafichwa, ila watu hawajajisumbua kuujua. Basi ni wajibu wako kuhakikisha kila mtu anajua ukweli huo na wale watakaofanyia kazi, wataweza kuwa na maisha bora sana.

Huduma iliyo kuu ni kuwasaidia watu kuujua ukweli, na hapo ulipo sasa kuna ukweli ambao wengi hawaujui, ifanye kuwa kazi yako kubwa kuhakikisha ukweli wote ambao watu hawaujui wanaujua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha