“Let us get used to dining out without the crowds, to being a slave to fewer slaves, to getting clothes only for their real purpose, and to living in more modest quarters.”
—SENECA, ON TRANQUILITY OF MIND, 9.3b
Siku mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi hii nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana kwetu na kwa wengine pia.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari MAHITAJI YA MSINGI NI MACHACHE…
Ni vyakula vya aina ngapi unahitaji kula ili kuwa na afya bora?
Ni mavazi ya aina ngapi unahitaji kuwa nayo ili uweze kusitiri mwili wako na kupendeza?
Ni vitanda vingapi unahitaji kuwa navyo ili kuwa na usingizi mzuri unapolala?
Ni magari mangapi unahitaji kuwa nayo ili kuweza kutoka eneo moja na kwenda eneo jingine?
Ukijiuliza, kutafakari na kupata majibu ya maswali hayo na mengine mengi kwenye mahitaji yako, utagundua kwamba mahitaji ya msingi ni machache sana, na yapo ndani ya kila mmoja wetu kuyafikia.
Lakini wengi wameishia kuwa watumwa wa madeni kwenye maisha yao, siyo kwa sababu ya mahitaji ya msingi, bali kwa sababu ya matumizi ya anasa.
Pale unapotaka kula mboga saba,
Pale unapotaka kila fasheni ya nguo isikupite,
Pale unapotaka kuwa na malazi ya kifahari,
Pale unapotaka kila toleo jipya la simu, kompyuta, tv au gari visikupite,
Hapo ndipo unapotengeneza utumwa wa maisha yako.
Tiba ya hili ni kujikumbusha mahitaji ya masingi kabisa na kuweka nguvu zetu kwenye hayo.
Hii haimaanishi kwamba huhitaji kabisa kuhangaika na yale ya ziada,
Na wala haimaanishi kwamba kuna ubaya wowote wewe kuwa na mahitaji ya ziada na ya anasa.
Una uhuru wa kuwa na chochote unachotaka, lakini hakikisha huweki mategemeo yako kwenye vitu hivyo.
Kazana kupata chochote unachotaka, lakini siyo kwa sababu ukiwa nacho ndiyo utakuwa na furaha au utaheshimika na wengine.
Kama huna furaha ukiwa na gari moja, nakuhakikishia hutakuwa na furaha ukiwa na magari kumi.
Kama watu hawakuheshimu ukiwa huna nyumba, kuwa na uhakika kwamba hawatakuheshimu hata ukiwa na nyumba tano.
Tujifunze kujitofautisha na vitu vya nje, tujijengee uhuru wetu wenyewe, kwa kuwa tayari kusimama na kuendelea na maisha yetu hata pale tunapokosa au kupoteza kile kinachoonekana ni kikubwa sana kwa wengine.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutokuruhusu mahitaji yasiyo ya msingi kukuvuruga. Siku ya kutengeneza uhuru wako kwa kuwa na utegemezi kwenye mahitaji machache.
#UhuruUpoKwenyeUchache #MahitajiYaMsingiNiMachache #FurahaInaanziaNdani
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1