Jua linawaka na kutawanya nguvu zake kwenye eneo kubwa. Nguvu hiyo inatupatia mwanga wenye manufaa makubwa kwenye maisha yetu.

Mwanga huo wa jua unapokusanywa na kuelekezwa eneo moja, unatoa nguvu kubwa yenye uwezo wa kuchoma na kuunguza kitu na hata kuzalisha umeme pia.

Nguvu ni ile ile ya mwanga, lakini inapotawanywa inakosa uwezo wa kufanya makubwa kama pale inapokuwa imelengwa kwenye eneo moja.

Hivi pia ndivyo tunavyopaswa kufanya kwenye nguvu za miili yetu, tunapaswa kuzipeleka eneo moja na siyo kuzitawanya kwenye maeneo mengi kwa wakati mmoja.

Unapochagua kufanya kitu, ambacho ni muhimu, basi weka akili yako na nguvu zako zote kwenye kitu hicho kimoja. Usiruhusu usumbufu wowote uingilie kwenye ufanyaji wako wa lile ambalo ni muhimu.

Ni bora kutenga nusu saa au saa moja ya kufanya kitu bila ya usumbufu, kuliko kufanya kitu hicho kwa masaa mawili huku ukiwa na usumbufu.

Siku hizi watu wamekuwa wanapima kazi kwa muda waliofanya na siyo kwa matokeo waliyozalisha. Na hili ndiyo limeshusha sana uzalishaji na ufanisi wa wengi. Kwa sababu mtu anafanya kazi masaa 10, huku akipokea simu, akijibu meseji, akitembelea mitandao ya kijamii na kusema amefanya kazi kweli. Katika masaa hayo 10, ukiangalia kwa kina, kazi hasa amefanya kwa masaa mawili.

Sasa unaonaje kama ukibadili ratiba yako ya siku, ukatenga masaa mawili ambayo utajifungia na kufanya kazi yako bila ya usumbufu wowote, kisha masaa nane yanayobaki ukaruhusu usumbufu wowote na kufanya chochote unachojisikia?

Lenga nguvu zako eneo moja kwa wakati na utapata matokeo bora kuliko kutawanya nguvu hizo kwenye maeneo mengi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha