“No, it is events that give rise to fear—when another has power over them or can prevent them, that person becomes able to inspire fear. How is the fortress destroyed? Not by iron or fire, but by judgments . . . here is where we must begin, and it is from this front that we must seize the fortress and throw out the tyrants.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 4.1.85–86; 87a

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii mpya tuliyoiona leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA .
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari LINDA NGOME YA NDANI DHIDI YA HOFU…
Roho yako ndiyp ngome yako ya ndani,
Hii inapaswa kulindwa dhidi ya maadui wanaoisaka ili waiangushe.
Kama ambavyo ngome za ufalme au ikulu za nchi zinalindwa, hivyo pia ndivyo unavyopaswa kulinda roho yako, ambayo inajumuisha imani yako na hisia zako.

Wale wanaotaka kuiangusha roho yako, huwa wana silaha kubwa mbili ambazo zina nguvu ya kuangusha imani na hisia zako.
Silaha hizo ni HOFU na TAMAA.
Watu huwa wanaibua hofu ndani yako kwa kukuonesha kwamba kuna kitu unakosa kama huchukui kitu fulani. Usipokuwa imara utaangushwa na hofu hizo. Angalia hata matangazo mengi, yanatumiwa watu wenye mwonekano mzuri na kukushawishi kwamba usipochukua kile wanachotangaza basi maisha yako yatakuwa mabaya. Hofu inakutawala na unaishia kununua kitu usichotaka.

Kwa upande wa tamaa, watu wamekuwa wanaibua hisia za kupata kitu kizuri kwa urahisi ndani yako. Na wewe ukikubali tamaa hiyo ikuingie basi wanakuangusha. Angalia mara zote ambazo umewahi kuibiwa, kutapeliwa, kupata hasara au kupoteza fedha. Kila wakati kuna tamaa iliwaka ndani yako. Watu walikuambia hii hapa ni biashara nzuri kufanya, ambayo hauhitaji kufanya kazi na faida unapata mara mbilibya fedha uliyoweka. Kwa akili za kawaida, akili imara unajua kabisa hicho kitu hakiwezekani, lakini unaoneshwa watu unaoambiwa wamefanikiwa sana kupitia biashara hiyo, unaona labda ni kweli, wacha ujaribu na hapo unakuwa umetengana na fedha zako milele.

Kama tukiweza kulinda ngome yetu ya ndani, roho na hisia zetu, na mara zote tukatumia vizuri akili zetu kufikiri kwa usahihi bila ya kuingiliwa na hofu au tamaa, tutafanya maamuzi bora mara zote na tutaepuka sana matatizo mengi tunayopitia.
Linda ngome yako ya ndani, tambua haraka pale wengine wanaoojaribu kuibua hisia ndani yako ili kunufaika na usikubali kunasa kwenye mitego hiyo.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kulinda ngome yako ya ndani ili isiangushwe kwa hofu na tamaa. Hakuna awezaye kukulazimisha uwenna hofu au tamaa, hivi ni vitu unavyoruhusu mwenyewe.
#LindaNgomeYaNdani #TawalaHisiaZako #FikiriKwaUsahihiMaraZote

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1