Kanuni nzuri ya kuendesha maisha yako ni sheria ya dhahabu, ambayo inasema watendee wengine vile ambavyo ungependa wakutendee wewe pia. Yaani kama kuna kitu ambacho hupendi wengine wakufanyie, basi na wewe usiwafanyie wengine.

Lakini kama ilivyo kwenye mambo mengi ya maisha, ni rahisi kusema kuliko kufanya. Na hii ni kwa sababu kuna vitu huwa tunavifanya kwa kutokujua kama vina madhara kwetu au kwa wengine.

Moja ya maeneo hayo ni muda, huwa tunathamini sana muda wetu na hatupendi watu waupoteze. Lakini cha kushangaza, sisi ni vinara wa kupoteza muda wa wengine.

Wengine wakipoteza muda wetu tunakasirishwa na kuwalalamikia, lakini kwenye kupoteza muda wa wengine hatufikirii hata mara mbili.

Na hili linatokana na hali kwamba sisi wenyewe ni wapotezaji wa muda wetu, hivyo kupoteza muda wa wengine siyo kitu kinachotusumbua, ni kama hatuoni kabisa.

Unaweza kupanga ratiba zako za mambo utakayoyafanya, lakini wakati wa kufanya unapofika huyafanyi, ukijifanyia hivyo wewe mwenyewe hujilaumu wala kuumia, lakini mwingine akikufanyia unaumia. Ndiyo maana inakuwa rahisi kwako kuwafanyia wengine, kwa sababu kujifanyia mwenyewe haikusumbui.

Sasa tunapaswa kuvunja hilo, tunapaswa kuanza kuheshimu muda wa wengine, na hilo litatusaidia kuheshimu muda wetu pia.

Kama umemwahidi mtu mtaonana kwa muda fulani, basi hakikisha kwa muda huo unapatikana kweli, unawahi kufika na kutekeleza kile ulichoahidi.

Kama unamwambia mtu una kitu muhimu kwake, basi hakikisha ni muhimu kweli, umuhimu ambao unaweza kufidia vitu vingine anavyoacha kwa wakati huo.

Unapokuwa na kazi ya mtu ya kufanya na ukamwahidi itakuwa tayari baada ya muda fulani, kazana uwezavyo ukamilishe ndani ya muda ulioahidi.

Na kama unapata nafasi ya kusema au kuandika kitu ambacho unataka watu wasikilize au kusoma, basi hakikisha ni kitu muhimu na kinachoongeza thamani kwenye maisha yao na siyo tu kitu cha kupoteza muda wao.

Kwa kila unachofanya kwa ajili ya wengine, jiulize je ninathamini na kujali muda wao? Kwa kuanza kufuatilia muda wa wengine hivyo, inakuwa rahisi kwako kufuatilia na kuthamini muda wako pia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha