Kama kuna neno moja lenye nguvu sana, neno linaloweza kukupa uhuru mkubwa na udhibiti wa muda wako basi ni neno HAPANA.
Lakini pia ni neno ambalo watu wengi huwa wanaogopa kulitumia, kwa sababu hatupendi kuwaangusha wengine, na hivyo tunajikuta tukisema NDIYO kwa baadhi ya vitu, ili tu kuwaridhisha wale wanaotaka, lakini ndiyo hiyo haitoki ndani yetu.
Sasa tumekuwa tunatumia sana ndiyo kwa kuangalia upande mmoja tu, upande wa kuwaridhisha wengine. Lakini kama tungeangalia upande wa pili, wa madhara ya ndiyo tunazotoa, tungekazana zaidi kutumia hapana.
Hapa tunakwenda kuiangalia vizuri hapana ili tuweze kuitumia kwa usahihi.
Mtu anapotaka kitu fulani kutoka kwako, na wewe ukamwambia HAPANA, maana yake umesema hapana kwenye kitu kimoja tu, kile ambacho mtu huyo alitaka.
Lakini mtu anapotaka kitu fulani kutoka kwako, na wewe ukamwambia NDIYO, maana yake umesema hapana kwa vitu vingine vyote kwa kukubali hivyo ambacho mtu huyo anataka.
Ina maana muda au umakini utakaoweka kwenye kile ulichosema NDIYO, huwezi kuutumia kwenye kitu kingine chochote, hivyo ni sawa na umesema HAPANA kwenye hivyo vitu vingine vyote.
Sasa swali linakuja kwako, kipi bora, kusema HAPANA kwa kitu kimoja au kusema HAPANA kwa kila kitu? Ukisema hapana umekataa kitu kimoja, ukisema ndiyo umekataa kila kitu. Ukisema hapana unaokoa muda wako wa baadaye, ukisema ndiyo inakugharimu muda wako wa baadaye. Kusema hapana ni akiba, kusema ndiyo ni mkopo.
Sema hapana mara nyingi uwezavyo, kama siyo kitu unachokubaliana nacho na unachokithamini sana na chenye manufaa makubwa kwako na kwa wengine, sema hapana na wala usione aibu. Utaokoa muda wako na kuutumia kwa yale ambayo ni muhimu zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,