Unapokuwa huna fedha, huwa unakuwa na ubunifu mkubwa sana. Unakuwa na umakini mkubwa sana kwenye kila unachofanya. Unaziona njia za gharama rahisi za kufanya vitu na hata njia za bure kabisa. Unakuwa na mawazo mazuri ya kutunza fedha kidogo uliyonayo na unaitumia kwa yale ambayo ni muhimu tu.

Kwa kifupi, unapokuwa huna fedha za kutosha, ubahili unakuwa ndiyo mtindo wako wa maisha, siyo kwa kuchagua, bali kwa sababu inakubidi kuishi hivyo. Anasa zinakuwa kitu cha mbali, ambacho hakikusumbui kwa sababu huna namna ya kuzimudu.

Unapokuwa huna fedha za kutosha unaweza hata kupata sifa kutoka kwa wengine, kwamba wewe ni mtu makini, mtu unayejali, mtu usiye na mambo mengi na sifa nyingine kama hizo.

Kwa kuanza na fedha kidogo, unajenga tabia hizo za kibahili ambazo zinakuwezesha kutunza vizuri kipato chako na kukiongeza zaidi. Sasa kipato chako kinapoongezeka ndiyo wakati hatari sana kwako.

Huu ni wakati ambao baadhi ya gharama ndogo ndogo zinaanza kukunyemelea kwenye matumizi yako. Ghafla unajikuta vile vitu ulivyojali sana mwanzoni kwa sasa huvijali tena, kwa sababu fedha ipo. Ghafla unaanza kupuuza gharama ndogo ndogo.

Kwa kifupi, pale uhaba wa fedha unapoondoka, unaona hustahili tena kuishi maisha ya ubahili. Unaona huna haja ya kujitesa juu ya vitu vidogo vidogo wakati fedha ipo.

Lakini mabadiliko haya ya jinsi unavyoichukulia fedha huwa hayakuachi salama. Hii ni kwa sababu gharama hizi nyemelezi huwa hazina ukomo, huwa zinaingia kidogo kidogo na kuendelea kukua kadiri muda unavyokwenda.

Gharama hizi huwa ni rahisi sana kuingia, lakini ni ngumu sana kuziondoa, kwa sababu kidogo kidogo unakuwa umeanza kutegemea vitu ambavyo siyo muhimu sana, lakini ukishaanza kuvitumia ghafla vinageuka na kuwa muhimu.

Unapaswa kuwa makini sana na gharama hizi nyemelezi, kuhakikisha haziingii kwenye matumizi yako. Haimaanishi kwamba ujitese, badala yake unapaswa kuwa na vipaumbele kwenye fedha zako na matumizi yako pia. Kwa sababu bila ya vipaumbele ghafla kila kitu kinageuka na kuwa muhimu zaidi. Hilo linapelekea gharama kuwa juu na hivyo kukurudisha nyuma kwenye mipango ya kifedha unayokuwa nayo.

Hii ni kwenye biashara na hata maisha binafsi. Kwenye biashara ni muhimu zaidi kwa sababu gharama nyemelezi huwa zinakuza matumizi ya biashara na kupunguza faida ambayo biashara hiyo inatengeneza. Na kwenye maisha binafsi, gharama nyemelezi zinapunguza akina unayojiwekea, lakini pia zinaiba muda wako, badala ya kuutumia kwenye mambo muhimu, unajikuta ukiutumia kwenye kuhangaika na gharama hizo nyemelezi.

Unapaswa kuwa na msimamo mzuri wa matumizi yako ya kifedha, uwe na msingi ambao unaufuata katika kufanya maamuzi ya kifedha, msingi utakaozuia gharama hizi nyemelezi zisiwe mzigo na hata kikwazo kwako kufanikiwa zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha