Kila mmoja wetu atakufa, hilo halina ubishi. Ambacho wengi wetu hatujui ni siku na saa ya tukio hilo kutokea.

Hivyo kwa kutokujua huko, watu wamekuwa wanapokea tofauti swala hilo la kifo.

Wapo ambao huona hakuna haja ya kujisumbua sana na maisha kwa sababu mwisho wa siku utakufa, hivyo hata ukijihangaisha kiasi gani, utakufa tu.

Wengine huona ndiyo nafasi ya kuishi maisha yasiyo na majukumu, maisha yasiyo ya kujituma na kujiumiza, kwa kujiambia hata kama watajitafutia mali au kufanya kazi sana, bado watakufa na hawataondoka na chochote.

Pia wapo ambao hutumia kifo kama sababu yao ya kujipa kila starehe hata kama ina madhara kwao. Mfano mtu anaweza kutumia vilevi ambavyo vinaharibu mwili wake, kwa kisingizio kwamba hata asipotumia vilevi hivyo bado tu atakufa.

Na wapo ambao huwa wakikumbuka kuhusu kifo wanapatwa na hofu kubwa, hofu inayowazuia kuchukua hatua kubwa ambazo walipanga kuchukua.

Sasa wote hao achana nao, tuje kwako, wewe unapokifikiria kifo, nini kinakuja kwenye fikra zako? Jiulize swali hilo na tafakari kwa dakika chache.

Kitu kimoja muhimu sana ambacho kifo kinapaswa kutukumbusha ni kufanya kitu sahihi kwa wakati sahihi. Kwamba kama kuna kitu tunachojali sana kufanya, basi tunapaswa kukifanya kwa usahihi na tunapaswa kukifanya sasa, siyo baadaye wala kesho, kwa sababu hujui nini kinakwenda kutokea.

Upo usemi weka mipango kama utaishi milele na chukua hatua kama utakufa kesho. Lengo ni moja, unapokumbuka kwamba siku moja utakufa, inapaswa kuwa msukumo wa wewe kuchukua hatua, ili usije ukaondoka hapa duniani hujaacha alama yoyote muhimu.

Usikitumie kifo kwa sababu nyingine yoyote ile isipokuwa kujisukuma kufanya kilicho sahihi kwa wakati sahihi. Na maisha yako yatakuwa bora zaidi kila siku.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha