“Nothing can satisfy greed, but even a small measure satisfies nature. So it is that the poverty of an exile brings no misfortune, for no place of exile is so barren as not to produce ample support for a person.”
—SENECA, ON CONSOLATION TO HELVIA, 10.11b
Ni siku mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tumeiona nafasi hii nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari MAHITAJI YAKO YA MSINGI NI MACHACHE…
Mahitaji yetu huwa yana tabia ya kukua kadiri tunavyopiga hatua kwenye maisha yetu.
Na kadiri mahitaji hayo yanavyokua, ndivyo tunavyoamini kwamba maisha yetu hayawezi kwenda bila ya mahitaji hayo.
Lakini huko ni kujidanganya,
Ukiangalia kwa umakini, mahitaji yako ya msingi ni machache sana.
Na wala sihitaji kutumia nguvu kubwa kukushawishi, bali nikukumbushe tu maisha yako ya nyuma.
Hebu kumbuka kipato chako cha kwanza wakati unaanza maisha ya kujitegemea, iwe ni mshahara au faida. Najua kilikuwa kidogo sana ukilinganisha na unachopata sasa. Je maisha hayakuenda?
Hebu jikumbushe nyumba uliyokuwa unakaa wakati unaanza maisha, kwa hakika ilikuwa ndogo kuliko unayokaa sasa, lakini maisha hayakusimama.
Kadhalika kwenye vitu vingine kama gari, mavazi, na mali nyingine.
Kadiri unavyopiga hatua kwenye maisha, ndivyo mahitaji yanavyoongezeka na inakuwa rahisi kuamini kwamba bila hayo yote maisha yako hayawezi kwenda.
Ukweli unaopaswa kujua ni kwamba, maisha yako yanaweza kwenda vizuri tu hata ukipoteza asilimia 90 ya kila ulichonacho sasa.
Na hii ni kwa sababu mahitaji yako ya msingi ni machache sana,
Na utayaelewa pale utakapolazimika kujibana kwenye huo uchache.
Unapoelewa kwamba mahitaji yako ya msingi ni machache, inakuweka huru, inakufanya uache kuwa mtumwa au tegemezi wa chochote kwenye maisha yako.
Na ukishakuwa huru, maisha yako yanakuwa bora sana.
Unapojua kwamba unaweza kupoteza karibu kila ulichonacho sasa na bado maisha yako yakaenda vizuri, hukosi usingizi kwa jambo lolote.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutambua mahitaji yako ya msingi ni machache na hivyo kuwa huru na kutokutegemea chochote kwamba kisipokuwepo maisha yako yatasimama.
#MahitajiYaMsingiNiMachache #HakunaUlichokosa #UsitegemeeVyaNjeYako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1