“If you lay violent hands on me, you’ll have my body, but my mind will remain with Stilpo.”
—ZENO, QUOTED IN DIOGENES LAERTIUS, LIVES OF THE EMINENT PHILOSOPHERS, 7.1.24

Ni jambo la kushukuru sana kwetu sisi ambao tumepata nafasi ya kuiona siku hii ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari USIRUHUSU YEYOTE AGUSE NGOME YA NDANI…
Tunajiambia kwamba tunaishi zama za uhuru, kwamba hakuna tena utumwa.
Lakini hili siyo kweli, utumwa wa kimwili umeondoka, lakini sasa kuna utumwa mkubwa na unaotesa sana, huu ni utumwa wa kiakili.
Watu wanakazana kudhibiti fikra zako na wakishazifikia basi huna ujanja tena mbele yao. Utafanya kile wanachotaka wao, huku ukijiambia kwamba umechagua wewe mwenyewe, kumbe wamecheza na akili yako.

Mfano mzuri ni pale mtu anapofanya kitu cha kukuudhi, kisha wewe ukapata hasira na kuchukua hatua ambazo zinamnufaisha mtu huyo na kukuumiza zaidi wewe.
Watu wakishajua ni rahisi kwako kupata hasira, au kuwa na furaha sana, wanakuweka kwenye mitego ya aina hiyo na wewe unaingia bila ya kujua.

Tulishajifunza kuhusu ngome yako kuu, ngome unayopaswa kuilinda wakati wote. Ngome hiyo ni fikra zako. Linda na kudhibiti fikra zako. Usimpe yeyote nafasi ya kupenyeza kwenye ngome hii. Usilazimishwe na yeyote kufikiri chochote.
Watu wanaweza kufanya chochote watakacho, wakakutukana, wakakupiga, wakakuibia, wakakufunga au kukutesa, lakini hayo yote yanafanywa kwenye mwili na hupaswi kuruhusu kabisa yaguse ngome yako ambayo ni fikra zako.

Kila wakati linda na dhibiti fikra zako,
Usiweke utegemezi wako kwa mtu au kitu chochote cha nje,
Usiruhusu wengine kucheza na fikra zako.
Na hata kama mambo ya nje yamevurugika kiasi gani, ukiendelea kutunza utulivu wako wa ndani, ukadhibiti fikra zako, mara zote utafanya maamuzi ambayo ni sahihi kwako.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kulinda na kudhibiti fikra zako dhidi ya wale wanaozinyemelea ili kuzitumia kwa manufaa yao.
#DhibitiFikraZako #UsitegemeeYaNje #KuwaNaUtulivuWaNdani

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1