“Everything turns on your assumptions about it, and that’s on you. You can pluck out the hasty judgment at will, and like steering a ship around the point, you will find calm seas, fair weather and a safe port.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 12.22
Kuiona siku hii nzuri sana ya leo ni bahati ya kipekee sana kwetu.
Siyo kila aliyepanga kuiona siku hii amepata nafasi hii.
Hivyo sisi ambao tumeipata hii nafasi, tunapaswa kuitumia vyema, kwa kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kila tunalofanya ili kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USIKIMBILIE KUHUKUMU…
Sisi binadamu ni viumbe wa kuhukumu.
Linapotokea jambo lolote, huwa tunakimbilia kutoa hukumu zetu kwa wale waliosababisha jambo hilo.
Labda ni mtu ameharibu kitu, tunahukumu moja kwa moja kwamba ni wazembe.
Labda ni mtu amepoteza kitu fulani, tunahukumu kwamba hawajali.
Labda umemsalimia mtu na hakuitiia, tunahukumu kwamba ana dharau.
Mara zote, hukumu hizi tunazozitoa haraka huwa siyo sahihi,
Huwa kunakuwa na sababu kubwa inayopelekea watu kufanya walichofanya na siyo ile ambayo tunakuwa tumejipa sisi wenyewe.
Hivyo basi ni wajibu wetu kuwapa watu nafasi kabla ya kuwahukumu.
Kujikamata sisi wenyewe wakati tunahukumu na kujizuia kuendelea na hukumu hiyo.
Kujua ya kwamba chochote unachofikiria kuhusu mtu mwingine kutokana na alichofanya siyo sahihi, mpaka utakapodhibitisha yeye mwenyewe bila ya mashaka yoyote kwamba amefanya kwa kukusudia.
Nje ya hapo wape watu nafasi,
Huenda mtu amefanya kwa kutokujua,
Huenda mtu amekosea kwa bahati mbaya,
Huenda mtu alielewa maelekezo vibaya,
Huenda mtu alifanya kwa nia njema asijue kwamba ni tatizo kwako.
Huenda mtu hakukusikia,
Huenda mtu hakukuona.
Ukianza na dhana hizi kabla ya kuhukumu, utakuwa tulivu zaidi na utapata nafasi ya kumsaidia mtu kuwa bora kuliko kuhukumu.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuepuka kuwahukumu watu haraka kabla ya kuwapa nafasi.
#UsikimbilieKuhukumu #SiyoKilaMtuAmekusudiaKukuumiza #UsijibebesheMizigoYaHukumu
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1