Kama unataka maisha yako yawe rahisi, kama unataka kuacha kuyafanya maisha kuwa magumu zaidi ya yanavyopaswa kuwa, basi usitake kushinda kila aina ya ubishani.
Kama kuna mtu amesema kitu ambacho hukubaliani nacho, siyo lazima uanze kubishana mpaka ushinde, kwa sababu unaamini wewe ndiyo uko sahihi zaidi. Tabasamu, tikisa kichwa na endelea na mambo mengine ya muhimu zaidi kwako.
Kwa kutumia mkakati huu, siyo tu utaokoa muda na nguvu zako, bali pia utaboresha sana mahusiano yako. Kwa sababu changamoto nyingi zinazotokea kwenye mahusiano, huwa zinaanzia kwenye ubishi wa kijinga jinga ambao wengi hupenda kuuendekeza.
Unakumbuka nilishakuambia wewe siyo kiranja wa dunia, wewe siyo msimamizi wa kuhakikisha kila mtu anafikiri, kusema na kufanya kilicho sahihi. Hivyo unapobishana na wale wasiokubaliana na wewe ni kama unalazimisha dunia nzima iwe kama unavyotaka wewe, kitu ambacho hakiwezekani hata kidogo. Hivyo kukifanya ni kuchagua kupoteza nguvu zako.
Maisha ni mafupi, jifunze kutokuruhusu kuvurugwa na vitu vidogo vidogo, kama huu ubishani wa mambo madogo madogo ambayo hayana umuhimu wowote kwenye maisha yako.
Waruhusu watu kuwa tofauti na wewe, waruhusu watu kukosea, waruhusu watu kuwa vile wanavyotaka na epuka sana kuingia kwenye ubishani usiokuwa na tija. Muda na nguvu zako zina matumizi bora sana kwako zaidi ya kubishana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,