Tunapoona watu wengine wanapiga hatua kubwa kuliko sisi, huwa tunakimbilia kujiambia kwamba watu hao wana bahati au wamekutana na upendeleo fulani ambao sisi hatujakutana nao.
Haya ni majibu ya kujifariji, pale ambapo wengine wanapiga hatua na sisi hatupigi.
Wakati mwingine tunakuwa watu wa kwanza kukosoa hatua wanazopiga wengine, japo ni hatua bora kuliko tunazopiga sisi, huwa hatukosi maneno ya kuweka, labda ni kwa namna wanavyofanya au vipaumbele ambavyo watu hao wanavyo.
Hatua zote hizi ambazo tumekuwa tunachukua kwa wale ambao wanapiga hatua kuliko sisi, zimekuwa hazitusaidii sisi kupiga hatua, badala yake zinatuacha pale tulipo sasa na wale waliopiga hatua wanaendelea kupiga hatua zaidi.
Kwa wale wenye mafanikio makubwa zaidi, wale watu ambao ni maarufu na wanajulikana na wengi, ndiyo kabisa wanapokea ukosoaji wetu kwa kiwango kikubwa. Mtaje mtu yeyote mwenye mafanikio makubwa na watu watakuambia madhaifu yake au makosa yake. Huwa tunajifariji sana pale tunapogundua kwamba wale waliopiga hatua kuliko sisi wana madhaifu au makosa fulani wanayoyafanya.
Lakini unapokuwa mtu wa kuangalia makosa na madhaifu ya wengine, hakuna kikubwa unachojifunza ambacho kitakusaidia na wewe upige hatua. Sana sana utajifariji kwamba wewe ni bora kitabia kuliko yule aliyekuzidi kwa mafanikio, kitu ambacho hakina msaada wowote kwako.
Njia bora ya kujifunza kwa wale waliofanikiwa, ili na wewe uweze kufanikiwa pia ni kujiuliza ni kitu gani watu hao wanajua, ambacho wewe hukijui kuhusu mafanikio? Ni hatua gani za tofauti wanazochukua, ambazo wewe huchukui katika safari ya mafanikio?
Ukijiuliza maswali haya, unaanza kuona vitu vya tofauti na ulivyozoea, unakuwa tayari kujifunza zaidi kupitia watu hao na hapo unakuwa kwenye nafasi ya wewe kupiga hatua zaidi.
Kila mtu ana madhaifu na makosa yake, acha kujifanya wewe ndiye hakimu wa dunia wa kuamua nani yuko sahihi na nani hayuko sahihi. Jukumu lako ni kujifunza yale mazuri ambayo watu wanayafanya na wanafanikiwa, ili na wewe uyafanye na kufanikiwa pia.
Ukiona mtu amefanikiwa kuliko wewe, jua kuna vitu vya tofauti anajua na kufanya ambavyo wewe hujui. Kuwa mnyenyekevu na jifunze vitu hivyo kwake na jifunze vitu hivyo kwake na wewe utaweza kupiga hatua kubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,