“There is no evil in things changing, just as there is no good in persisting in a new state.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 4.42

Ni siku mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi nyingine ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari MABADILIKO SIYO MABAYA NA WALA SIYO MAZURI…
Huwa tunapenda kujiambia kwamba mabadiliko ni mazuri,
Lakini tunajiambia hivyo kama njia ya kujifariji, kwa sababu huwa hatuyapendi mabadiliko.
Lakini kutokuyapenda kwetu mabadiliko hakubadilishi chochote.
Mabadiliko yataendelea kutokea.
Na kutokea kwa mabadiliko siyo kuzuri wala kubaya, ni kitu ambacho kinatokea.
Hivi unaweza kusema kuchomoza au kuzama kwa jua ni kuzuri au kubaya? Huwezi kusema hivyo, kwa sababu ni kitu kinachotokea kila siku.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa mabadiliko.

Ubaya au uzuri wa kitu ni tafsiri yetu sisi wenyewe.
Ukiacha kuweka tafsiri zako kwenye vitu na ukavipokea kama vinavyokuja, utaacha kujiumiza na mambo mengi yanayoendelea kila siku.
Kujiumiza au kujifariji na matokeo hakuna msaada wowote kwako.
Bali kuyapokea mabadiliko na kuyatumia vizuri ndiyo kutaweza kukusaidia sana.

Ukawe na siku bora ya leo, siku ya kuyapokea mabadiliko na kuyatumia vizuri katika safari yako ya mafanikio.
#KilaKituKinabadilika #YapokeeMabadiliko #YatumieMabadilikoVizuri

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1