Kama unataka kufanikiwa, unapaswa kuwa mnyenyekevu na msikivu, na kisha kuwa tayari kujifunza kutoka kwa wengine na kuchukua hatua kwenye maisha yako. Kama kuna kitu chochote ambacho wengine wameweza kufanya, hata wewe unaweza kukifanya kama utakuwa na maarifa sahihi na kuweka juhudi za kutosha.
Lakini watu wengi wamekuwa wanajizuia kujifunza na hata kukua kwa kuona kile ambacho wengine wanafanya kinafaa kwa hao wengine lakini siyo kwao wao.
Unawaangalia au kuwasoma wale ambao wamefanikiwa wakieleza njia walizopita mpaka wakafanikiwa halafu unajiambia hiyo inawezekana kwao, lakini siyo kwako wewe, kwa sababu hali yako ni tofauti.
Huko siyo tu kujidanganya, bali kujizuia kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako. Hakuna chochote kinachowezekana kwa wengine halafu kishindikane kwako, hakipo. Chochote kitashindikana kwako kama wewe mwenyewe umeamua kishindikane, lakini siyo kwa sababu ya hali fulani ya tofauti ambayo wewe unayo.
Ukiacha ujuaji na ubishi, ukawa tayari kujifunza na kuchukua hatua, huwezi kubaki hapo ulipo sasa, lazima utapiga hatua kubwa. Ukiacha kupingana na yale ambayo wengine wanakushirikisha, na kuchagua kuyaamini na kuyafanyia kazi, lazima utapiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.
Amua sasa kuwa mnyenyekevu na msikivu na kuwa tayari kujifunza na kuchukua hatua. Kila ambacho wengine wamefanya wakafanikiwa, amini kinaweza kufanya kazi kwako pia, jifunze na fanyia kazi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,