“Don’t allow yourself to be heard any longer griping about public life, not even with your own ears!”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 8.9

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana kwetu.
Tumeipata nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari HATA MASIKIO YAKO YASISIKIE…
Tunaposema hupaswi kulalamika, wengi huwa tunafikiri ni yale malalamiko na lawama tunazotoa kwa wengine.
Hivyo tunaweza kuacha hizo, lakini tukaendelea kulalamika na kujilaumu sisi wenyewe.

Lakini hilo pia halisaidii,
Kujilalamikia na kujilaumu wewe mwenyewe hakuna msaada mkubwa kwako,
Bali kunakufanya ujione ni wa chini, usiyefaa na usiyeweza.
Kwa chochote kinachotokea au kutokutokea unapaswa kuchukua hatua sahihi kwa wakati huo.
Na siyo kulalamika au kujilaumu kwa namna yoyote ile.
Hata kama yapo makosa uliyoyafanya, jifunze na kusonga mbele, kuendelea kujikumbusha makosa hayo kila mara haina msaada wowote kwako.

Hata masikio yako mwenyewe hayapaswi kusikia lawama na malalamiko yako.
Muda wako ni wa thamani mno kuupoteza kulaumu na kulalamikia chochote kile.
Kama kuna jambo hulipendi basi chukua hatua za kulibadili,
Na kama huwezi kulibadili nasi achana nalo, lipotezee na endelea na mambo mengine.
Hiyo ndiyo kanuni rahisi ya kuwa na maisha tulivu ambayo kila siku unapiga hatua na kuwa bora zaidi.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutolalamika wala kulaumu hata kwako wewe mwenyewe. Siku ya kuchukua hatua sahihi kwa lolote linalotokea ili kusonga mbele.
#Usilalame #Usilaumu #ChukuaHatua

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1