“When philosophy is wielded with arrogance and stubbornly, it is the cause for the ruin of many. Let philosophy scrape off your own faults, rather than be a way to rail against the faults of others.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 103.4b–5a
Hongera sana mwanamafanikio kwa nafasi hii nyingine nzuri tuliyoiona leo.
Na nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USIHUKUMU, ISHI MAISHA YAKO…
Unapojifunza falsafa, unapokazana kuwa bora, unapojituma ili kufanikiwa zaidi, lengo kuu ni wewe kuyaishi maisha yako, na siyo kuwahukumu wengine.
Kwa kujua misingi ya falsafa ni rahisi kuona wengine hawayajui maisha,
Kwa kukazana kuwa bora ni rahisi kuona wengine hawana uwezo kama wako.
Kwa kujituma na kufanikiwa zaidi ni rahisi kuona wale ambao hawajafanikiwa kama wewe ni wazembe.
Yote hayo ni kuhukumu, kitu ambacho siyo sahihi kwako kufanya.
Unachopaswa kukazana ni kuyaishi maisha yako, na kuwaacha wengine wayaishi maisha yao.
Usiwe mtu wa kuhukumu, usiwe mtu wa kuwapima wengine na wewe,
Usiwe mtu wa kutaka kila kitu kiende kama unavyotaka wewe, kila mtu awe kama ulivyo wewe.
Kipimo sahihi cha ukomavu wetu kama watu ni kuweza kuyaishi maisha yetu na kuwaacha wengine wayaishi maisha yao bila ya kuwahukumu.
Unaweza kuwashauri namna bora zaidi, unaweza kuwapa mwongozo, lakini hupaswi kuwahukumu.
Hili ni jambo muhimu sana la kutafakari na kuliishi kila siku, kwa sababu zama tunazoishi sasa ni zama za kila mtu kujiona yupo sahihi na wengine wote wamekosea.
Wewe badili hilo, kuwa kwako sahihi haimaanishi ambao hawafanyi kama wewe wanakosea.
Wewe kazana kuyaishi maisha yako, na waache wengine wayaishi maisha yao.
Wewe siyo kiranja wa dunia, jipumpumzishe na hangaika na yako.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kukazana kuyaishi maisha yako na kuwaacha wengine waishi maisha yao bila ya kuwahukumu.
#Usihukumu #IshiMaishaYako #WaacheWengineWaishiMaishaYao
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1