Watoto na wanyama wanafanana kwa kitu kimoja, huwa wanachukua hatua kutokana na hisia ambazo wanazo kwa wakati huo. Ndiyo maana tunaweza kuwatega na kuwakamata wanyama. Pia ndiyo maana ni rahisi kuwalaghai watoto.

Lakini watu wazima wanaofikiri kwa usahihi, huwa wanatenda na kisha kutengeneza hisia kutokana na matendo yao. Hawaanzi na hisia kwanza, bali wanaanza kwa fikra, wanachagua nini wanataka kufanya, kisha kupitia kufanya hicho, wanatengeneza hisia wanazotaka kuwa nazo.

Kwa njia hiyo ya kutenda bila kuongozwa na hisia, ndiyo wengi wameweza kufanya makubwa, wameweza kuwa na utulivu katika hali mbalimbali na kutengeneza matokeo bora sana.

Lakini wapo watu wazima wengi ambao wamekuwa wanaendesha maisha yao kama watoto au wanyama, wanaruhusu hisia zao ndiyo ziwasukume kuchukua hatua. Sasa ukishajikuta unasukumwa kuchukua hatua kwa hisia, jua utakosea, jua matokeo yoyote utakayoyapata hayawezi kuwa bora.

Jizue sana kusukumwa na hisia, badala yake sukumwa na fikra, panga kila unachofanya na katika kukifanya ndiyo unaweza kutengeneza hisia unazozitaka wewe.

Inachukua muda kujijengea mfumo huu bora wa kuchukua hatua bila ya kusukumwa na hisia, inahitaji kuweza kuisimamia na kuitumia vizuri akili yako. Weka kazi kwenye hili na utaweza kuondokana na matatizo na changamoto nyingi unazoingia kutokana na kuchukua hatua kwa kusukumwa na hisia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha