“If you’ve seen the present, you’ve seen all things, from time immemorial into all of eternity. For everything that happens is related and the same.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 6.37
Tushukuru na kufurahi kwa kuiona siku hii mpya.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari HAKUNA KIPYA KINACHOTOKEA…
Kila kitu kinachotokea leo, kilishatokea tena huko nyuma, na kitaendelea kutokea tena siku zijazo.
Haijalishi unakiona kipya au cha kushangaza kiasi gani, jua hakina upya, huenda kimekuja kwa namna tofauti.
Dunia imekuwa inaenda hivi nyakati zote, watu wanazaliwa, wanakua, wanaumwa, wanapata ajali, wanakufa, wanafanya kazi, wanagombana, wanapendana, jua linachomoza, linazama, mvua inanyesha, majanga yanajitokeza na kuendelea.
Kujua hili kuna maana na msaada mkubwa sana kwetu,
Kwanza hatutashangazwa na chochote kitakachotokea, kwa sababu tunajua siyo kipya.
Pili tunaweza kujifunza kwa wengine, ambao wamepitia yale tunayopitia na kujua jinsi ya kukabiliana nayo.
Tatu hatutamezwa na shauku ya kutaka kesho ifike kwa kuwa tunafikiri itakuwa tofauti, badala yake tutaiishi leo kwa ukamilifu, tukijua yanayotokea leo ndiyo yatakayotokea kesho pia.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuishi kwa ukamilifu, ukijua hakuna jipya linalotokea, hivyo kupokea kila kitu kwa utayari na kuiishi leo vizuri na siyo kuruhusu matamanio ya kesho kuiharibu leo yako.
#HakunaKipyaKinachotokea #JifunzeKutokaKwaWengine #IshiVizuriLeo
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1