Kadiri maendeleo yanavyotokea kwenye sayansi na teknolojia, ndiyo mfumo wa elimu unavyozidi kuachwa nyuma.
Mfumo huu wa elimu unaotumika sasa, umeweka mkazo mkubwa kwenye kukariri yale ambayo mtu anapaswa kuyajua na ambayo atakwenda kuyatumia kwenye kazi zake.
Hili lilikuwa muhimu kipindi cha nyuma, ambapo haikuwa rahisi kupata maarifa na taarifa pale mtu anapozihitaji, hivyo mtu kuwa amekariri yale mambo muhimu, ilisaidia sana.
Lakini kwa sasa, maendeleo ya sayansi na teknolojia, yamefanya kutafuta taarifa kuhusu kitu chochote kuwa rahisi kuliko kufikiria wewe mwenyewe. Mfano ukiandika na kutafuta kitu kwenye mtandao wa google, chini ya sekunde moja utapata majibu mengi sana.
Kwa kuwa ni rahisi kupata maarifa na taarifa, kukariri hakuna tena matumizi, ni kujichosha na kutumia vibaya akili zetu.
Kwa hiyo ina maanisha kwa kuwa kila mtu anaweza kugoogle hakuna tena haja ya kusomea taaluma mbalimbali? Kwamba kwa kuwa kila mtu anaweza kugoogle ugonjwa wake na akapata majibu hakuna tena haja ya watu kusomea udaktari?
Jibu ni hapana, haja ya kusomea taaluma hizi ipo na ni kubwa sana. Kwa sababu kinachohitajika siyo kuweza kutafuta, bali kujua ni nini unatafuta na utakifanyia nini.
Hivyo lazima watu waendelee kusomea taaluma hizi, lakini msisitizo ubadilike, utoke kwenye kukariri na kwenda kwenye kuelewa na kufanya maamuzi.
Yaani msingi mkuu wa kusomea taaluma yoyote ile uwe ni kumwezesha mtu kufanya maamuzi sahihi kwa nyakati mbalimbali anazokuwa anapitia. Na hapo mtu ataweza kutafuta maarifa na taarifa kwa wakati anapozihitaji na kuzitumia kufanya maamuzi sahihi.
Muhimu ni kuweza kufanya maamuzi sahihi na siyo kuwa umekariri vitu vingi. Ukiweza hili, elimu yoyote utakayokuwa umepata itakuwa na manufaa kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,