“Let us prepare our minds as if we’d come to the very end of life. Let us postpone nothing. Let us balance life’s books each day. . . . The one who puts the finishing touches on their life each day is never short of time.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 101.7b–8a
Kuiona siku hii nyingine mpya na nzuri sana kwetu ni bahati ya kipekee kwetu.
Siyo kwa akili zetu wenyewe, wala nguvu zetu, bali ni kwa bahati tu.
Na njia pekee ya kushukuru na kulipa bahati hii, ni kuiishi siku hii vyema, kufanya yale ambayo ni muhimu kwetu na kwa wengine pia.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari ISHI LEO KAMA NI SIKU YAKO YA MWISHO…
Una mipango muhimu sana ambayo umejiwekea kufanya siku ya leo, lakini huifanyi, unaiahirisha na kujiambia utafanya kesho! Kwa sababu gani? Kwa kuwa umejishawishi kwamba kesho lazima utakuwepo. Vipi kama ungeambiwa leo ndiyo siku yako ya mwisho hapa duniani? Je ungeahirisha yale uliyopanga kufanya?
Unachagua kufanya mambo yanayopoteza muda wako na yasiyokuwa na mchango wowote kwako wala wale wanaokuzunguka. Na hii yote ni kwa sababu unajua bado muda unao, kesho pia ipo. Kama ungeambiwa leo ndiyo siku yako ya mwisho, je ungepoteza muda kwa yale unayopoteza muda sasa?
Leo una nafasi ya kuwaambia watu wa karibu kwako unawapenda, una nafasi ya kuwasiliana na wale watu muhimu kwako. Lakini hutafanya hivyo, kwa sababu utajiambia uko bize na kesho ipo ya kufanya hivyo. Vipi kama leo ingekuwa ndiyo siku ya mwisho kwako, bado ungesema uko bize kwa hilo muhimu kiasi hicho?
Rafiki, ukweli ni kwamba kuna siku itakuwa ya mwisho kwako, na ubaya ni kwamba hujui siku hiyo ni lini. Inaweza kuwa leo, inaweza kuwa kesho, au mwaka kesho au miaka 10 au 50 ijayo. Lakini ipo siku.
Ili kutokujisahau na ili kutokupoteza muda kwa yale yasiyo muhimu, ishi kila siku yako kama vile ndiyo siku ya mwisho kuwa hapa duniani.
Na hufanyi hivyo kwa maana ya kula starehe kwa sababu umefikia mwisho, bali unafanya hivyo kwa maana ya kumilisha yale muhimu kabisa kabla hujaondoka hapa duniani.
Nafasi unayo leo rafiki, hebu iishi kama ndiyo siku yako ya mwisho, kwa kuhangaika na yale muhimu pekee na kuachana na yasiyo muhimu.
Hivi ukijua unakufa leo, utakuwa na muda wa kumkasirikia mtu au kuwa na kinyongo? Sasa kwa nini ufanye mambo kama hayo leo?
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuishi kama vile ndiyo siku yako ya mwisho hapa duniani, na hivyo kuhangaika na yale muhimu pekee. Na huenda ikawa hivyo, kwa sababu hakuna ayakayekikwepa kifo.
#IshiLeoKamaSikuYaMwisho #KazanaNaYaliyoMuhimu #UsiahirisheChochote
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania