Kwenye kila jambo unalofanya kwenye maisha yako, kuna njia mbili mbele yako. Kuna njia ndefu, ambayo ndiyo sahihi, lakini ngumu na yenye changamoto nyingi. Halafu kuna njia fupi ambayo ni ya mkato, rahisi lakini isiyo sahihi.

Kwa kuwa binadamu hatupendi ugumu, wote huwa tunashawishiwa kujaribu njia ya mkato, kwa kuamini inaweza kuwa tofauti au kutupa kile tunachotaka. Hakuna ubaya kwenye kujaribu hilo, ila tu ujaribu ukiwa unajua unakwenda kujifunza kwamba njia ya mkato haifanyi kazi na hata ikifanya kazi haileti matokeo uliyotarajia.

Na unapokwenda kutumia njia ya mkato jua hili, kama huna muda na nguvu za kutosha kufanya kitu kwa usahihi, kwa njia ndefu, basi usipoteze muda wako kukifanya kwa njia ya mkato. Kwa sababu matokeo utakayoyapata kwa njia ya mkato yatakulazimu urudi kufanya kwa njia ndefu, hivyo kama huwezi, ulichofanya kwa njia ya mkato kimepotea.

Weka vipaumbele vyako kwa usahihi, kwa kila unachotaka kukifanya, jiulize kama kweli kina manufaa kwako na kama kweli una muda na nguvu za kutosha kuwekeza kwenye kitu hicho ili uweze kupata matokeo mazuri. Kama majibu ni hapana, usijaribu hata kutumia njia ya mkato, maana utakuwa umechagua kupoteza muda na nguvu kidogo ulizonazo kwenye jambo lisilo na manufaa yoyote kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha