“For it’s disgraceful for an old person, or one in sight of old age, to have only the knowledge carried in their notebooks. Zeno said this . . . what do you say? Cleanthes said that . . . what do you say? How long will you be compelled by the claims of another? Take charge and stake your own claim—something posterity will carry in its notebook.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 33.7
Ni siku nyingine mpya,
Siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Na msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kuzingatia maeneo hayo matatu, siku hii ya leo itakuwa bora na ya kipekee sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JENGA HOJA ZAKO…
Ni jambo la aibu sana kukutana na mtu mzima ambaye umri umekwenda lakini kila anachoongea ni kile alichosoma au kusikia kwa wengine.
Kila hoja aliyonayo ni amesoma kwa mwandishi fulani au kwenye kitabu fulani.
Hili siyo sahihi kabisa,
Kadiri umri wako unavyokwenda, unapaswa kujenga hoja zako na kuzisimamia na siyo kutegemea hoja ulizojifunza kwa wengine.
Una uzoefu ambao tayari umeshaupata, una thamani kubwa mno.
Kwa miaka uliyoishi kuna hekima ambayo umejijengea, ina thamani pia.
Sasa ni wakati wa wewe kujenga hoja zako, kupitia uzoefu ulionao na hekima uliyojijengea.
Toa hoja mpya, ambazo umezifikiria wewe na watu wazipokee na kuziishi.
Toa hoja zako kwa maneno na hata matendo pia.
Hutaacha alama hapa duniani kwa kusambaza hoja za wengine, bali utaacha alama kwa hoja mpya utakazoleta na zikawa na mchango kwa wengine.
Ni rahisi kusema Socrates alisema hivi, au Plato alisema hivi, au Nyerere alisema hivi. Kila mtu anaweza kusema hivyo.
Tunachotaka kusikia ni wewe unasema nini?
Kwa uzoefu ulionao mpaka sasa na hekima ambayo umejijengea, unaamini na kusimama upande gani kwenye jambo fulani?
Jenga hoja zako, na zisimamie, hicho ndiyo kitakutofautisha na wengine.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujenga hoja zako na kuzisimamia kutoka kwenye uzoefu ulionao na hekima uliyojijengea. Usikubali kuwa shabili wa hoja za wengine, ni wakati sasa wa kujenga hoja zako.
#UnaHojaGani #UnasimamiaNini #DuniaInatakaKukusikia
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani
http://www.t.me/somavitabutanzania