Kilicho mbele yako sasa ndiyo kitu muhimu kuliko vyote kwenye maisha yako.
Ukiweza kuweka umakini wako wote kwenye hicho kilicho mbele yako sasa, utaweza kufanya makubwa sana.
Tatizo watu wengi wamekuwa wakipotezwa kwa kuruhusu umakini wao kuhama kutoka pale walipo sasa.
Wengi huruhusu umakini wao kwenda kwenye wakati uliopita, kwenye vitu walivyofanya huko nyuma ambavyo hawawezi kuvibadili kwa namna yoyote ile. Pia wamekuwa wanaruhusu umakini kwenda kwenye mambo yajayo, ambayo bado hawajayafikia.
Usiruhusu hili, wewe weka umakini wako wote kwenye kile unachofanya sasa, kile kilichopo mbele yako sasa. Unasoma makala hii, weka umakini wako wote hapa, acha kufikiria yaliyopita, acha kuhangaika na yajayo, weka umakini wako wote kwenye hiki unachofanya sasa. Kwa namna hii unaweza kuelewa kwa undani na kuchukua hatua sahihi.
Kama unafanya kazi, weka umakini wako wote kwenye kazi unayofanya, weka simu mbali, achana na mitandao ya kijamii na acha kuzurura mitandaoni. Ukiweka dakika chache za umakini kwenye kazi na utatoa matokeo mazuri kuliko kuweka masaa mengi huku ukikosa umakini.
Moja ya mabadiliko madogo unayoweza kufanya kwenye maisha yako na yakaleta matokeo makubwa sana ni hili la kuweka umakini wako wote kwenye kile unachofanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,