Kwenye kila hali unayopitia au kukutana nayo kwenye maisha yako, unakuwa na machaguo mawili mbele yako.

Chaguo la kwanza ni kitu rahisi kufanya, hili utaliona haraka. Ni kile ambacho kinakuwa rahisi kwako kufanya, hakikuumizi wala kukusumbua, ndiyo ambacho kila mtu anafanya. Lakini kilicho rahisi kufanya, mara nyingi huwa kinazalisha matatizo makubwa zaidi, huwa hakileti matokeo mazuri.

Chaguo la pili ni kitu sahihi kufanya. Hiki ndiyo kilicho sahihi kufanya kwa hali unayokuwa unapitia. Ni kitu kigumu kufanya na ambacho wengi wanakwepa kufanya. Lakini kufanya kilicho sahihi kunaleta matokeo mazuri na hakutengenezi matatizo mapya.

Mfano, kipato chako hakitoshelezi, kitu rahisi kufanya ni kwenda kukopa fedha ili utimize mahitaji yako. Ni rahisi, unazipata fedha na kutimiza mahitaji yako. lakini hapo umezalisha tatizo jipya, tatizo la madeni ambalo litakuwa mzigo mkubwa sana kwako, kwani utalipa ulichokopa pamoja na riba. Kitu sahihi kufanya kwenye hali hii ni kuwa tayari kukosa unachohitaji kwa muda huku ukikazana kuongeza kipato chako. Njia hii siyo rahisi, utakuwa unajitesa na kujinyima, itakuhitaji kujisukuma zaidi, lakini mwisho wa siku italeta matokeo bora, kipato chako kitaongezeka huku ukiwa huna madeni.

Rafiki, kila unapojikuta njia panda, jiulize njia rahisi ni ipi na njia sahihi ni ipi, kisha chukua njia sahihi na achana na njia rahisi. Kama inakuwa vigumu kwako kujua njia sahihi ni ipi, angalia kile ambacho wengi wanafanya, kisha usifanye hicho, maana wengi hupenda kufanya kilicho rahisi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha