Kila mtu kwenye maisha kuna mbio ambazo anashiriki, na kila mtu anayo nafasi ya kushinda zile mbio ambazo amechagua kushiriki. Kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni aina ya mbio ambazo mtu amechagua kushiriki.
Kuna aina kuu ya mbio kwenye kila eneo la maisha yetu.
Aina ya kwanza ni mbio za kuelekea kileleni, hizi ni mbio za kuwa bora na kupiga hatua zaidi kujitofautisha na wengine. Ushindi wa mbio hizi unakupa mafanikio makubwa. Unashiriki mbio hizi pale unapofanya kazi kwa utofauti na kutoa thamani kubwa, pale unapofanya biashara kwa upekee na kuwapa wateja huduma ambayo hawawezi kuipata sehemu nyingine. Mbio hizi ni ngumu, lakini ushindi wake una manufaa makubwa kwa anayeshiriki.
Aina ya pili ni mbio za kuelekea chini, hizi ni mbio za kukazana kuwa kawaida, kufanya kile ambacho kila mtu anafanya na kutokuchagua kujitofautisha kwa namna yoyote ile. Ushindi wa mbio hizi unakupelekea kushindwa kwenye jambo unalofanya. Unashiriki mbio hizi pale unapofanya kazi kwa mazoea na uvivu, kuwategea wengine na kuyakimbia majukumu, kwenye biashara mbio hizi unazishiriki pale unapoiga wengine wanafanya biashara gani, pale njia pekee unayotumia kuvutia wateja ni kupunguza bei kuliko wengine. Mbio hizi ni rahisi kushiriki, lakini ushindi wake unakugharimu sana kwa sababu unakuondoa kabisa kwenye mchezo.
Kabla hujaendelea na mbio ulizopo sasa, hebu jipe muda na kujiuliza je ni mbio zipi unazoshiriki. Je ni mbio za kwenda kileleni au mbio za kwenda chini? Chagua mbio sahihi kwako ili usifike kwenye ushindi na kushangaa matokeo unayopokea.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,