“To bear trials with a calm mind
robs misfortune of its strength and burden.”
—SENECA, HERCULES OETAEUS, 231–232

Ni siku nyingine mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi hii nzuri sana kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kuzingatia maeneo hayo matatu, siku hii ya leo itakuwa bora na ya kipekee sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari YASHINDE MAGUMU NA MAJARIBU…
Kwenye maisha, utakutana na magumu na majaribu mbalimbali,
Mengine yatakuwa madogo kama changamoto za kazi, biashara au mahusiano.
Na mengine yatakuwa makubwa kama magonjwa, kesi na hata kukabiliana na kifo.

Magumu na majaribu haya yamekuwa yakiwavuruga wengi, wakiona hawakustahili kupitia hayo na kujiona ni dhaifu na wasioweza kupambana nayo.
Lakini wewe usikubali kirahisi,
Kwa sababu ndani yako una nguvu kubwa ya kukabiliana na magumu na majaribu yoyote utakayoyapitia.

Nguvu hiyo ni kuwa na utulivu wa akili wakati unapopitia magumu na majaribu.
Usitaharuki na kuanza kulaumu au kulalamika.
Badala yake tuliza fikra zako, ona ni wapi ulipo sasa na njia ipi bora ya kutoka hapo au kuenda na hali hiyo kama kutoka haiwezekani.
Unapoweza kuwa na utulivu wa akili katika nyakati za magumu na majaribu, yanakosa nguvu kabisa.
Hata wale ambao wanaweza kuwa wamekutengenezea magumu na majaribu hayo, wataumia sana wakiona una utulivu wa akili.
Yaani walitengeneza magumu hayo ili wewe uumie, lakini utulivu wako unawafanya wao waumie zaidi.

Kuwa na utulivu wa akili wakati wa changamoto, magumu na hata majaribu ni nguvu ambayo kila mmoja wetu anayo.
Anza kuitumia sasa na utakuwa na maisha bora na yasiyoyumbishwa na chochote.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa na utulivu wa akili pale unapopitia magumu na majaribu ili kuyanyima nguvu.
#DhibitiFikraZako #UsiyumbishweNaChochote #KilaKituKinapita

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania