Ipo kauli kwenye Biblia kwamba kilicho dhaifu hakitauona ufalme wa mbinguni.

Kauli hii imepewa msisitizo zaidi na mwanabaiolojia Charles Darwin aliyeweza kujionea maisha ya viumbe mbalimbali na kugundua kwamba, viumbe dhaifu huwa hawaishi muda mrefu. Aliona kwamba kwenye mazingira yoyote yale kuna ushindani, na katika ushindani huo, viumbe dhaifu ndiyo hushindwa haraka. Aliita dhana hii survival of the fittest, yaani walio imara ndiyo wanaopona.

Rafiki, hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mafanikio, hakuna aliye dhaifu ambaye atayaona mafanikio. Kama ambavyo tunajifunza kila siku, safari ya mafanikio siyo rahisi, siyo lele mama, ni safari ngumu, yenye vikwazo na changamoto nyingi sana, hakuna aliye dhaifu ambaye ataweza kuvuka vikwazo na changamoto hizo.

Hivyo rafiki yangu lazima uwe imara mno, na uimara wako unapaswa kuwa kwenye maeneo matatu muhimu.

Lazima uwe imara kwenye mwili, kwa sababu mwili wako utahitaji kujisukuma na kufanya kazi zaidi ya ulivyozoea, bila ya mwili imara, hutaweza aina ya kazi unayopaswa kufanya ili kufanikiwa. Uimara wa kimwili unajenga kwa kula kwa afya, kufanya mazoezi na kupata muda wa kupumzika.

Unapaswa kuwa imara kwenye akili, kuwa na maarifa bora, kujua kwa kina kila kitu kuhusu kazi au biashara yako na kuweza kufanya maamuzi bora ndani ya muda mfupi. Kama haupo imara kwenye akili, utaishia kutapeliwa, kufanya maamuzi mabovu na kuzidiwa na wale wanaojua kuliko wewe. Uimara wa kiakili unajengwa kwa kulisha akili yako maarifa sahihi kupitia usomaji vitabu na kupata maarifa mengine.

Na muhimu kabisa, unapaswa kuwa imara kiroho, kwa sababu safari hii inakatisha tamaa, utakutana na vikwazo mbalimbali, wengine watakuangusha, kuna wakati utaona kama dunia nzima inakucheka wewe, lakini hizo ndizo nyakati unazopaswa kuwa imara sana, na ukiwa imara kiroho utaweza kuvuka changamoto zote hizo. Uimara wa kiroho unajengwa kwa kuwa mtu wa imani, kusali na kufanya tahajudi.

Maisha ni magumu, mafanikio ni magumu, hakuna kilicho dhaifu ambacho kitaweza kufanikiwa kwenye haya maisha. Hakikisha wewe hauwi dhaifu, kuwa imara kimwili, kiakili na kiroho na hakuna kitakachoweza kukuzuia kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha