“We are all like children who first repeat the unquestionable “truth” told to us by our grandmothers, then the “truth” told to us by our teachers, and then, when we become older, the “truth” told to us by prominent people.” —After RALPH WALDO EMERSON

Kuiona siku hii mpya ya leo ni bahati ya kipekee sana kwetu.
Siyo kwa nguvu zetu, wala akili zetu, bali ni kwa neema.
Tuitumie siku hii vyema ili tuweze kufanya makubwa.

Kama unaendesha maisha yako kwa ukweli wa kuambiwa na wengine, basi huenda huna maisha.
Hii ni kwa sababu pamoja na njia njema ya wale wanaotuambia ukweli tunaopaswa kuishi nao, huwa wana ajenda zao binafsi, hivyo huwa wanaupindisha ukweli huo ili uendane na ajenda zao.

Ukiwa mtoto wazazi wanakupa ukweli usiohojiwa, wa jinsi ya kuishi maisha yako. Kwa kuwa wazazi wanataka utii wako na hawataki uumie, basi ukweli wanaokupa huwa wanaupindisha kidogo.
Mfano watakuambia usichukue hatua za hatari, usitake kuwa tofauti na mengine kamw hayo.

Unapoendelea kukua unapokea ukweli mwingine kutoka kwa walimu, ambao nao wanahitaji ushirikiano na utii wako ili kazi yao iwe rahisi.
Hivyo ukweli wao nao unapindishwa kidogo, wanakuahidi vitu ambavyo hawana uhakika navyo.
Hapa ndipo unapopata ahadi kama soma kwa bidii, faulu na utakuwa na maisha mazuri. Unapokea kama ukweli usiohojiwa na kuendesha maisha yako hivyo.

Unapokuwa mtu mzima, ambaye unaendesha maisha yako, unapokea ukweli kutoka kwa watu maarufu na viongozi pia. Hawa nao kwa sababu ya ajenda zao binafsi, wanaupindisha ukweli ili uwape ushirikiano wako. Hapa ndipo unapoambiwa ukinunua kitu fulani au ukiwa na kitu fulani utapata furaha. Unaambiwa ukimchagua fulani kuwa kiongozi basi maisha yako yatakuwa bora sana.

Rafiki, kama hivi ndivyo unavyoyaendesha maisha yako mpaka sasa, kwa ukweli wa kuambiwa na wengine, basi huna maisha yako, bali unaiga maisha ya wengine.

Unapaswa kuutafuta ukweli wa maisha yako wewe mwenyewe.
Hili ni jukumu ambalo huwezi kumpa mwingine na akalifanya kwa manufaa yako.
Kila mtu kuna namna ataupindisha ukweli ili anufaike.

Kwa kila ambacho wengine wanakuambiam usikimbilie kukubaliana nacho, bali kihoji.
Hoji kila unachokutana nacho, hoji kila unachoambiwa, hoji kila ambacho umekuwa unaamini sasa.
Na maswali muhimu ya kuhoji ni; je ni kweli? Na je kuna ushahidi gani wa kudhibitisha hilo?
Dadisi kila unachoambiwa kupata ushahidi ambao unadhibitisha au kupingana na kitu hicho.

Ukweli wa kweli ni ule unaoutafuta kwa jasho lako mwenyewe.
Kama unakubaliana na kila unachoambiwa na wengine kama ndiyo ukweli usiohijiwa, basi umekuwa unaishi maisha ambayo siyo yako.

Siku ya leo na kila siku kazana kuujua ukweli wa kweli kwa kuhoji na kudadisi kila kitu.
Uzuri tunaishi kwenye zama za maarifa na taarifa hivyo unaweza kujua chochote unachotaka kujua.
Tumia fursa hii vizuri ili kuupata ukweli kamili wa maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania