Kama kuna kitu ambacho hukitaki kwenye maisha yako, kupingana nacho ni njia ya uhakika ya kuendelea kuwa nacho. Hii ni kwa sababu unapopingana na kitu unakipa nguvu na hivyo kinakua zaidi.
Na hili liko wazi, fikiria kwenye maisha yako mwenyewe, huenda kuna kitu watu walikuwa wanakutania nacho, iwe ni jina fulani walikuwa wanakuita au kitu fulani ulikosea na hivyo kuwa utani kwako. Kadiri ulivyowakataza watu wasikutanie, ndivyo walivyozidi kukutania. Kadiri unavyowapinga na hata kukasirika kwa wao kukutania, ndivyo walivyozidi kukutania. Lakini baadaye ukaja kupuuza utani wao, ukaacha kujali na ghafla watu hao nao wakaacha utani huo.
Ni jambo la kushangaza, unapopambana na kitu ili kukikomesha kinakua zaidi, lakini unapoachana nacho kinapotea kabisa. Lakini hivyo ndivyo maisha yalivyo, kile unachokipa umakini wako ndiyo kinachokua zaidi. Kile unachokipuuza kinakosa nguvu na kufa.
Hivyo kama kuna kitu ambacho hukitaki kwenye maisha yako, usijisumbue kupambana nacho, utakipa nguvu zaidi. Badala yake chagua kukipuuza, na utaona jinsi kinavyokosa nguvu kabisa na kupotea chenyewe.
Hili linakwenda mpaka kwenye tabia binafsi, kama kuna tabia ambayo inakusumbua kubadili, ukihangaika nayo ndiyo inazidi kuwa ngumu kwako. Hivyo njia sahihi ni kuipuuza.
Mfano kama una tatizo la kukosa usingizi unapokwenda kitandani, ukikazana kujiambia lazima upate usingizi hutaupata, lakini ukienda kitandani na kujiambia hujali kuhusu usingizi, wewe unajiweka kitandani ukiwa tulivu na utashangaa muda mchache baadaye usingizi umekujia.
Mara nyingi tumekuwa tunazua vile tunavyovitaka kwa mahangaiko yetu wenyewe, tunakazana kufanya vitu ambavyo vinaweka ugumu zaidi kwenye kile tunachotaka. Mara nyingi kupuuza, hasa kwa yale tusiyoyataka, kuna nguvu kubwa ya kuyaondoa kuliko kupambana nayo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,