Fedha siyo kila kitu, lakini inahusika karibu kwenye kila kitu kwenye maisha yetu, hivyo kujitenga na fedha ni vigumu sana, hasa kwa maisha ambayo tumeshayazoea.

Kitu ambacho kinatupeleka kwenye msingi muhimu wa kuzingatia inapokuja kwenye matatizo na fedha.

Kama una tatizo ambazo fedha inaweza kutatua basi huna tatizo, bali tatizo ni huna fedha. Pata fedha, tatua tatizo na maisha yako yataendelea.

Hivyo badala ya kukaa chini na kujiumiza kwa tatizo ambalo fedha ingeweza kutatua, tumia muda huo kupata fedha ili uweze kutatua tatizo hilo.

Ukifikiri kwa namna hii, hakuna kinachoweza kukurudisha nyuma, kwa sababu mara zote utajua ni nini unapaswa kufanya.

Na vipi kama una tatizo halafu fedha haiwezi kutatua? Uachie muda, fedha ikishindwa basi muda ndiyo suluhisho kamili. Baada ya muda tatizo hilo litapotea au wewe utapotea. Kwa sababu tunajua hakuna kinachodumu milele.

Sijui kama unaelewa kile ambacho nataka uelewe leo, maana hakihusu fedha wala hakihusu tatizo, bali kinakuhusu wewe.

Ninachosema ni hiki, kuna sababu ya kusumbuliwa na kitu chochote kwenye maisha yako. Kwa sababu tatizo au changamoto yoyote unayopitia inaweza kutatuliwa na fedha au haiwezi kutatuliwa. Kama inaweza kutatuliwa basi tafuta fedha. Kama haiwezi kutatuliwa uachie muda.

Kila siku unapaswa kupeleka muda na nguvu zako kwenye kufanya yale muhimu kwako na siyo kusumbuka na matatizo ambayo huwezi kuyatatua kwa kuyahofia au kuyafikiria sana.

Pata fedha, zitatatua matatizo yako mengi, na yale ambayo hayawezi kutatuliwa na fedha basi yape muda.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha