Kuna watu ambao wanajaribu kufanya mambo mabaya kwako na unaweza kuwaona ni watu wabaya na wakatili sana.
Lakini watu hao unapaswa kuwaonea huruma kuliko unavyowaona wabaya.
Mtu yeyote anayetaka kukuumiza, jua ya kwamba na yeye anaumizwa.
Mtu yeyote anayetaka kukutesa, jua kwamba pale alipo naye anateseka.
Mtu ambaye anataka kuyavuruga maisha yako, jua maisha yake nayo yamevurugwa.
Watu ambao hawajakomaa kiroho wanapopitia hali ngumu, huwa naona siyo sawa wapitie hali hizo peke yao, hivyo hutafuta wengine wa kuhakikisha wanapitia hali sawa, na wale wa karibu kwao ndiyo wanaoingia kwenye mtego huo.
Kuwa makini sana na kwepa mtego wa aina hii, usikubali kuingia kwenye kile ambacho mtu anakutengenezea ili uwe kama yeye.
Unapoona mtu anafanya kitu ambacho lengo lake ni kutengeneza ubaya au ugumu kwako, yachunguze maisha yake na utaona kuna mabaya na magumu yanaendelea kwake.
Ukishajua hilo, utaishia kuwaonea huruma badala ya kuwalalamikia na kuwalaumu kwa wanayotaka kufanya.
Pia utaona hatua sahihi za kuchukua, kama unaweza kuwasaidia kuvuka ugumu huo, au unapaswa kukaa nao mbali, hasa kama ugumu huo umeshaondoa ule utu ndani yao.
Na kwa upande wako binafsi, jichunge sana pale unapopitia ubaya au ugumu usiupeleke kwa wengine. Ni asili ya binadamu kufanya hivyo, hakikisha unajizuia usiingie kwenye hilo. Kama kuna chochote kibaya au kigumu unapitia, kitatue na siyo kutaka wengine nao wawe nacho, haina msaada kwako wala kwao.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,