Mpumbavu yeyote anaweza kuyafanya mambo kuwa magumu (compicated), inahitaji akili kuyafanya mambo kuwa rahisi (simplified).

Chochote unachofanya, chochote unachojihusisha nacho, kifanye kiwa rahisi kwako na kwa wengine kukielewa.

Unapotaka kuwashawishi watu kwa jambo lolote lile, lifanye kuwa rahisi kueleweka na watu hao.

Siku za nyuma ilionekana ujanja ni kufanya mambo yaonekane magumu, lakini zama hizi, ujanja ni kuyafanya mambo kuwa rahisi.

Watu hawawezi kuchukua hatua kama mambo yanaonekana kuwa magumu, wanahitaji kuelewa ndiyo waweze kuchukua hatua.

Hivyo ni muhimu sana, wewe mwenyewe kuelewa kwa kina kile unachofanya kabla hujajaribu kumweleza mwingine.

Lazima wewe mwenyewe uwe umeshawishika kabla hujajaribu kumshawishi mtu mwingine.

Yafanye mambo kuwa rahisi na utaokoa muda na nguvu zako ambazo ungepoteza kuelezea mambo magumu na kuzipeleka kwenye kufanya yaliyo muhimu zaidi.

Zoezi muhimu sana unalopaswa kufanya ni hili, ili kujua kama kweli unakielewa kitu kwa urahisi, pata picha unamwelezea mtoto wa darasa la tano kwa namna ambayo atakuelewa. Au unamwelezea mzee wa miaka 80 na aweze kukuelewa. Kama chochote unachofanya au unachojihisisha nacho huwezi kuwaelezea watu hao wawili wakakuelewa, basi wewe mwenyewe hujakielewa na umekifanya kuwa kigumu.

Yafanye mambo kuwa rahisi, ni njia bora ya kuyaelewa na kuwashawishi wengine pia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha