Unapopanga kuingia kwenye biashara mpya au kukuza zaidi biashara unayofanya sasa, lazima kuna mabadiliko unapaswa kuyafanya kwa ajili ya wengine.
Sasa kuna aina mbili za mabadiliko unayoweza kufanya.
Aina ya kwanza ni kubadili namba ambavyo watu wamekuwa wanapata kile ambacho wanakitaka. Hapa hubadili wanachotaka, bali unabadili namna wanavyokipata. Unaweza kukiboresha zaidi, wakakipata kwa urahisi zaidi au haraka zaidi. Aina hii ni rahisi, wateja wanakuelewa na wengi huwa wanaitumia. Mfano simu mpya ambazo zinatoka kwa sasa, ni mabadiliko ya namna watu wanapata kile ambacho wanakitaka.
Aina ya pili ni kubadili kile ambacho watu wanataka, hapa unaleta kitu kipya kabisa kwa watu, kitu ambacho hawajawahi kujua kama wanakitaka na kisha kuwafanya wakitake. Hii ni njia ambapo unakuja ua ugunduzi au uvumbuzi mpya ambao watu hawajawahi kuutumia. Njia hii ni ngumu, wale unaowalenga hawailewi na inachukua muda kukubalika na wengi. Mfano toleo la kwanza la simu janja (smartphone), lilibadili kabisa kile ambacho watu wanakitaka.
Kujua aina hizi mbili kunakusaidia kufanya maamuzi kwenye biashara yako au chochote unachofanya. Unapaswa kujua ni wakati gani wa kubadili namna watu wanapata wanachotaka au kubadili kabisa kile wanachotaka. Kama ndiyo unaanza biashara kabisa, ni vyema kuanza na aina ya kwanza, kama upo kwenye biashara na unataka kuitofautisha zaidi, basi fanya mabadiliko ya aina ya pili.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,