Kuna vitu kwenye maisha yako unaweza kuvichukulia poa sana wakati unavyo, huoni umuhimu wake mkubwa.
Ila pale unapovikosa vitu hivyo, ndiyo unagundua kwamba vilikuwa muhimu sana kwako.
Na wakati huo unapogundua, unakuwa umeshachelewa.
Kabla ya kufika kwenye hali hiyo ya kugundua umuhimu wa kitu kwa kukikosa, anza kuthamini kila ulichonacho sasa.
Hata kama ni kidogo na cha kawaida kiasi gani, kithamini.
Unapokuwa na afya nzuri unaweza kuchukulia kitu cha kawaida, tena ukaenda mbali zaidi na kuchukua hatua za kuhatarisha afya hiyo. Ni mpaka pale unapopoteza afya hiyo ndiyo unagundua umuhimu mkubwa wa afya.
Mahusiano yote uliyonayo na wengine, ni muhimu sana kwako. Kuna wakati unaweza kuona watu wapo na mahusiano hayo hayahitaji kazi, ni mpaka pale yanapovunjika au unapompoteza mtu ndiyo unajua alikuwa muhimu kiasi gani kwako.
Thamini kila ulichonacho wakati unacho, huku ukijikumbusha kwamba hakuna kinachodumu milele, hivyo hupaswi kuchukulia kitu chochote kawaida.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,