Moja ya vikwazo vikubwa kwa wengi kujifunza na kupiga hatua kwenye maisha yao ni ujuaji.
Wengi huamini tayari wanajua kila wanachopaswa kujua hivyo hawana haja ya kujifunza tena. Na hapo ndipo wanapokuwa wamejichimbia kaburi na kujizuia kupiga hatua.
Hatua ya kwanza unayopaswa kuchukua ni kukiri kwamba kuna vitu vingi hujui, ukilinganisha unachojua na usichojua, unachujua ni tone kwenye bahari.
Kujua hivi siyo kwa lengo la kujidharau na kujikatisha tamaa kwamba hujui, bali kuwa mnyenyekevu na kujifunza.
Mifano ya hili iko wazi, watu waliofanikiwa mara zote huwa ni watu wa kujifunza, utawakuta wana vitabu vingi wanavyosoma, wanahudhuria semina na mafunzo mbalimbali na wanapokuwa kwenye mafunzo hayo wanajifunza kweli, hata kama ni kitu ambacho walishajifunza tena.
Lakini wale ambao hawajafanikiwa, huwa hawana muda wa kusoma vitabu au kuhudhuria semina na mafunzo mbalimbali. Watakuambia bila aibu kwamba mafunzo hayo hayana jipya, mambo ni yale yale ambayo tayari wanayajua.
Hapo ndipo utakapojiuliza kama kweli wanajua kama wanavyodai kujua, mbona hawana mafanikio makubwa?
Rafiki, jiwekee msimamo huu, kama mtu mwingine amepiga hatua ambayo wewe hujapiga, basi anajua kitu ambacho wewe hujui, na huwezi kujua kitu hicho kama hutakuwa tayari kujifunza.
Kuwa tayari kujifunza, kwa sababu hujui ambacho hujui mpaka pale utakapojua. Kujifunza ndiyo njia pekee ya kujua ni vitu gani hujui ili kuweza kuvijua. Kama unaamini unajua kila kitu, basi jua hujui.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,