Ni yale ambayo yanatokana na asili yako wewe, na siyo yale unayoiga kwa wengine.
Kama hujanielewa vizuri hapo namaanisha kile unachofanya ambacho kinaendana na asili yako, ndiyo kinachoweza kukupa wewe mafanikio ya kudumu.
Kile ambacho unapata msukumo mkubwa kutoka ndani yako kufanya, kile unachokipenda na kukijali sana, kiasi kwamba uko tayari kukifanya bure kabisa kama hakuna aliye tayari kukulipa.
Katika safari yako ya mafanikio, utakutana na wengi ambao watakuambia kama unataka kufanikiwa fanya hivi au vile, fanya kile ambacho mimi nimefanya na fanya kama nilivyofanya mimi.
Unaweza kufanya na ukapata mafanikio makubwa, lakini mafanikio hayo hayatadumu. Kwa sababu unahitaji nguvu kubwa kulinda mafanikio hayo, kitu ambacho kitakushinda wakati fulani na utaishia kupoteza mafanikio hayo.
Lakini pale mafanikio yanapotokana na asili yako, yanapotokana na kile kilichopo ndani yako, huna haja ya kutumia nguvu kulinda mafanikio hayo, kwa sababu yanakuwa ni sehemu yako.
Swali ni je utajuaje asili yako? Na utawezaje kuitumia kufanikiwa zaidi?
Jibu ni angalia ni kitu gani unapenda sana kufanya, kisha jiulize unawezaje kuongeza thamani kwenye maisha ya wengine katika kufanya kitu hicho, kisha kifanye, kwa viwango vya juu mno.
Wakati unakifanya, tengeneza njia ya watu kukulipa kupitia wewe kufanya kitu hicho na kazana kuwafikia wengi zaidi. Msukumo wako wa kwanza siyo fedha wala mafanikio, bali kutoa kile kilichopo ndani yako na kufanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Na hapo ndipo utakapojitengenezea nafasi ya kufanya makubwa na kufanikiwa sana, mafanikio ambayo yatadumu na wewe, kwa sababu hutachoka kufanya ulichochagua kufanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,