Kuna mstari kwenye biblia unaosema njia ya kuelekea kwenye uzima ni nyembembe, yenye miba na ngumu kupita. Lakini njia ya kuelekea jehanamu ni pana, iliyorembwa na rahisi kupita.
Mstari huu umebeba ukweli kuhusu maisha, ukweli ambao ukiujua, utakuwa na maisha bora sana.
Kwamba kile ambacho ni muhimu kwako kufanya, ambacho kitakuwa na manufaa kwako, siyo rahisi, kitakuwa kigumu na chenye changamoto nyingi. Lakini kile ambacho siyo muhimu, ambacho hakina manufaa kwako, kitakuwa rahisi na kitakuvutia sana kukifanya.
Hivyo basi, kila unapokuwa njia panda, na upande mmoja kuna kitu rahisi kufanya, huku upande wa pili kukiwa na kitu kigumu kufanya, mara zote chagua kulicho kigumu. Chagua kisichovutia, ambacho wengi wanakikwepa, lakini kilicho sahihi.
Kwa kuchagua hicho, kwanza unakuwa umepunguza ushindani, maana wengi hawapendi kufanya vitu vigumu. Pili kitakusukuma wewe uwe bora zaidi ya ulivyokuwa, katika kukabiliana na ugumu huo. Na tatu, kitakufikisha kwenye mafanikio makubwa, ambayo ndiyo unayataka.
Hakuna ambaye amewahi kuwa na mafanikio makubwa hapa duniani kwa kufanya vitu rahisi, ambavyo wengine wanavifanya. Mara zote watu wanafanikiwa kwa kufanya vitu vigumu ambavyo wengi hawapo tayari kuvifanya.
Chagua kilicho kigumu na pambana nacho bila ya kukata tamaa au kurudi nyuma, na ugumu huo utakubadilisha kabisa wewe na kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,