Kazi haziwaridhishi watu, watu hawafurahii kazi zao, watu wanahangaika kujaribu vitu vipya kila mara, watu hawafanikiwi.

Kwa sababu hawafanyi kazi hizo kwa ajili yao, bali wanazifanya kwa ajili ya wengine au kile ambacho wanategemea kukipata.

Mtu anachagua kufanya kazi au biashara fulani kwa sababu wengine wamemwambia ndiyo nzuri kufanya, au ndiyo ya hadhi yake au ndiyo inaheshimiwa zaidi na wengine.

Wengine wanachagua kufanya kazi au biashara kwa sababu ndiyo inalipa zaidi, wanajua kufanya hivyo ndiyo njia nzuri ya kufika kwenye utajiri na uhuru wa kifedha.

Kinachotokea ni watu wanaotumia vigezo hivi viwili kuchagua biashara au kazi, wanakosa upendo kwenye kazi hiyo, wanakosa msukumo mkubwa kwenye kufanya kazi hiyo na mwisho wanakosa furaha kwenye kile wanafanya na maisha kwa ujumla.

Kuondokana na hali hii, fanya kazi au biashara unayoifanya kwa sababu ndiyo kitu umechagua kufanya, na unajua mchango mkubwa unaotoa kwa wengine kupitia kile unachofanya. Usiangalie nani anafanya au unapata nini, angalia kwanza ni mchango gani unaoutoa kupitia kazi hiyo.

Kisha fanya, na unapomaliza kufanya, nenda hatua ya ziada. Weka mikakati ya juu, jisukume kufanya zaidi, toa thamani kubwa zaidi kwa wengine. Msukumo pekee wa wewe kufanya ni kwa sababu unataka kufanya, unataka kutoa mchango wako kwa wengine.

Kwa kusimama kwenye msingi huu, utapata vyote unavyotaka, sifa kutoka kwa wengine, kipato kikubwa, kuridhika na kufurahia unachofanya na maisha kwa ujumla.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha