Mtu akija kwako na kukuambia kuna fursa ya kupata fedha nyingi kwa haraka na bila ya kufanya kazi, cheka, kisha achana naye na nenda zako. Usijibizane naye, usibishane naye, wewe cheka na nenda na yako. Akikuuliza kwa nini unacheka mjibu umefurahi, kisha endelea na mambo yako.
Kwa nini ufanye hivi? Kwa sababu unajua kabisa kwamba hakuna pesa sahihi ambayo imewahi kupatikana kirahisi, kwa wingi na bila ya kufanya kazi.
Pesa ni zao la ung’ang’anizi, huwezi kuipata kirahisi na bila ya kuweka juhudi. Na hata ukiipata kwa namna hiyo, haitakaa na wewe muda mrefu, itakuhama na kwenda kwa wale ambao ni ving’ang’anizi.
Hii ni kanuni ya asili, huwezi kwenda kinyume nayo na ukabaki salama. Angalia kwa kila kiumbe, ni ung’ang’anizi pekee unaompa kile anachotaka. Simba pamoja na ukali na nguvu zake, swala hawajileti wenyewe kwake, ni lazima awinde, avizie, akimbize mpaka pale swala anapochoka na yeye kumkamata na kupata kitoweo. Simba hatatoa tu amri kwamba wewe swala hapo njoo uwe kitoweo kwangu, badala yake atapambana mpaka kumpata swala.
Okoa muda wako na nguvu zako, acha kuhangaika na vitu vipya kila siku, chagua eneo ambalo unalipenda na unalikubali, kisha weka ung’ang’anizi mpaka upate kile unachotaka. Hakuna njia nyingine isipokuwa hiyo. Na yeyote anayekuja kwako akikuahidi njia rahisi kuliko hii, kuna mawili; anataka kukutapeli au yeye mwenyewe hajui.
Wewe unajua vyema, hakuna njia ndefu kama njia ya mkato. Weka ung’ang’anizi na asili itakupa unachotaka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,