Hapo ulipo sasa ndiyo sehemu sahihi ambayo unapaswa kuwepo. Japokuwa siyo sehemu unayoweza kuwa unataka kuwa, lakini bila ya kuanzia hapo ulipo sasa, huwezi kufika kule unakotaka kufika.
Kile unachofanya sasa, ndiyo kitu muhimu kuliko vitu vingine vyote duniani. Japokuwa kinaweza kisiwe ndiyo kitu unachopenda kufanya, lakini bila ya kufanya hicho unachofanya sasa vizuri, huwezi kufika kwenye kile unachopenda kufanya.
Ukielewa hayo mawili, utakuwa na maisha bora, tulivu na yenye mafanikio makubwa.
Tunapotea pale tunapodharau pale tulipo sasa na kuona tunachofanya siyo muhimu.
Kumbuka kila dakika ya maisha yako ina thamani kubwa sana, hivyo hakikisha haipotei kwa namna yoyote ile.
Kufanya hivyo, anza kujali hapo ulipo sasa, haijalishi ndiyo ulitaka kuwepo hapo au la, wewe pajali, na patumie kufika kule unakotaka kufika. Hakuna mtu ambaye amewahi kujikuta juu ya kilele cha mlima kwa muujiza, bali kila mtu huanzia chini na kupiga hatua moja baada ya nyingine na hatimaye anafika kwenye kilele.
Chochote unachoruhusu mikono yako ishike, ndiyo kitu muhimu zaidi, weka mawazo yako yote, umakini wako wote na mapenzi yako yote kwenye kufanya kitu hicho. Usiruhusu usumbufu wa aina yoyote ukuingilie katika kufanya kile ambacho umepanga na kukubali kufanya.
Kuwa pale unapokuwa, mawazo yako yawe yamezama kwenye kile unachofanya na usiruhusu hofu au fikra zozote kuingilia utulivu wako. Kwa kufanya hivi tu, tayari unajipa utulivu mkubwa, unakuwa bora na utafika kwenye mafanikio makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,